Na Allan Kitwe, TimesMajira Online, Tabora
MWENGE wa Uhuru umezindua mradi wa maji safi ya bomba uliogharimu zaidi ya sh mil 600 katika Kijiji cha Kigandu, kata ya Mwakashanhala Wilayani Nzega Mkoani hapa ambao umewezesha wananchi zaidi ya 6,000 kuanza kunufaika.
Akitoa taarifa ya utekelezaji mradi huo kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Godfrey Mnzava, Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Wilayani humo Mhandisi Gaston Ntulo amesema kuwa mradi huo umemaliza kilio cha muda mrefu kwa wakazi wa Kijiji hicho.
Amefafanua kuwa jumla ya fedha iliyotumika katika mradi huo ni sh mil 610.9 ambapo kati ya hizo sh mil 126.7 ni gharama ya ununuzi wa mabomba na kiasi cha sh mil 484.3 zimelipwa kwa mkandarasi Kampuni ya EDM Network Ltd.
Amebainisha kuwa mradi huo ni sehemu ya upanuzi wa mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria, ulioanza kutekelezwa Aprili 12, 2023 na kukamilika Mei 16, 2024 hivyo kumaliza kero iliyokuwa ikiwakabili wakazi wa Kijiji hicho na Vitongoji vyake.
Mhandisi Ntulo amefafanua kazi zilizofanyika katika utekelezwaji mradi huo kuwa ni pamoja na ujenzi wa tanki kubwa la maji lenye ujazo wa lita 150,000 na Ofisi 2 za Vyombo vya Watoa Huduma ngazi ya jamii za UBUKI na UMWAI.
Kazi nyingine ni ujenzi wa chemba 25, vituo vya kuchotea maji (dp)10, ununuzi wa bomba, uchimbaji wa mitaro na ulazaji wa bomba zenye urefu wa km 22.9, ununuzi wa pikipiki 2, komputa mpakato 1 na mashine ya kuprinti (printer) 1.
Ameongeza kuwa mradi huo umekamilika kwa asilimia 100 na upo kwenye muda wa matizamio na tayari wananchi wapatao 106 wameshaunganishiwa maji nyumbani kwao na bei ya maji kwa ndoo 3 ni sh 100 katika vituo vya kuchotea.
‘Tunamshukuru sana Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea fedha za kutosha kwenye utekelezaji wa miradi huo, hakika mama amesikia kilio cha wakazi wa Kata hii, amemaliza kero yao’, amesema.
Akizungumza baada ya kukagua na kuzindua mradi huo, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Godfrey Mnzava amesema kuwa mradi huo ni matokeo ya kazi nzuri inayofanywa na Rais Samia ya kuwatua akinamama ndoo kichwani.
Amepongeza kazi nzuri iliyofanywa na Wakala wa Maji (RUWASA) Wilayani humo kwa kusimamia vizuri mradi huo na kukamilika kwa wakati hivyo kuwezesha wananchi kuanza kunywa maji safi na salama ya bomba.
Aidha ametoa wito kwa wakazi wa Kijiji hicho na Wilaya nzima kuendelea kutunza mazingira na kulinda vyanzo vya maji ili kutoathiri upatikanaji huduma ya maji katika maeneo yao.
More Stories
Polisi yaonya vyama vya siasa
Mzumbe yaanika siri ya shahada udaktari wa heshima kwa Samia
Kujenga ofisi ya kisasa,akipewa ridhaa ya Uenyekiti