Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Dodoma
KAMPUNI ya Imara Tech imeleta ukombozi kwa wakulima nchini baada ya kuja na teknolojia ya kupukuchua (kubugusa) aina tisa za mazao ikiwemo mahindi, hivyo kumuondolea usumbufu na muda mrefu mkulima wakati wa kupukuchua mazao hayo.
Hayo yamesemwa kwenye Maonesho ya Nanenane kimataifa yaliyofanyika Viwanja vya Nzuguni mkoani Dodoma, na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Imara Tech Alfred Chengula,wakati anamueleza Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule, namna teknolojia hiyo ilivyorahisisha shughuli za mkulima.
“Imara Teknolojia ni kampuni ya kizawa ipo mkoani Arusha, na sisi tunajishughulisha na uzalishaji wa mashine za kilimo kwa ajili ya wakulima wadogo wadogo,tumekuja Nanenane kwa ajili ya kuwaonesha wakulima bidhaa tulizonazo, na moja ya bidhaa ambayo tumewaletea wakulima ni mashine pendwa ambayo ni ya kupukuchua na kukula mazao aina tisa tofauti.
“Kwamba ni mashine moja, lakini ina uwezo wa kupiga mazao tofauti tofauti kama vile mahindi, maharage, mtama, mbaazi, alizeti na mengineyo,mashine hii ni ndogo na ina uwezo wa kubebeka na pikipiki kutoka sehemu moja kwenda nyingine na kumrahisishia mkulima kuweza kujiongezea kipato pale ambapo ataweza kutoa huduma kwa wakulima wengine” alisema Chengule.
Chengula amesema mpaka sasa wameshahudumia wakulima 1,050, na wameweza kusambaza mashine hizo kwenye mikoa yote ya Tanzania na nje ya nchi, ambapo wanahudumia nchi nane (8) ikiwemo Burundi, Malawi, Rwanda, Zambia, Kenya, Uganda na Kongo DRC.
Mkuu wa Mkoa, Senyamule, alisema azma ya Rais Dkt. Samiia Suluhu Hassan amepanga kuwaaminisha Watanzania kuwa kilimo hakina msimu na hiyo ni kutokana na kujenga mabwawa makubwa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji, ambapo wakulima wataweza kulima na kuvuna mazao yao kwa uhakika.
“Katika Maonesho haya ya Nanenane kitaifa, tunaendelea kushuhudia mapinduzi makubwa kwenye Sekta ya Kilimo kwa kuwa na vifaa vya kilimo ili kuweze wakulima kufanya shughuli zao kwa kutumia teknolojia na utaalamu zaidi badala ya kutumia nguvu na mikono,haya ni mapinduzi makubwa, na yanaungana moja kwa moja na mipango ya Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutaka ile kilimo ni Uti wa Mgongo, iwe kwa vitendo.
“Wao wakulima wenyewe wanaendelea kujua umuhimu wa kutumia vifaa vya kisasa katika Sekta ya Kilimo. Tumeshuhudia wadau wakiamini na wakiungana na Serikali kuhakikisha wakulima wanapata teknolojia, na leo tunaziona jitihada za kumuunga mkono Rais” alisema Senyamule.
More Stories
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili
ACT-Wazalendo,waitaka Polisi kutobeba chama kimoja