November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Prof. Mkumbo aahidi barabara ya Makoka-Mchichani kujengwa kwa lami

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji na Mbunge wa Jimbo la Ubungo Prof. Kitila Mkumbo ameahidi kuwa barabara ya Mchichani – Makoka yenye urefu wa KM. 4.04 itajengwa kwa kiwango cha Lami kupitia mradi wa DMDP.

Akiwa katika Mkutano wa hadhara kwenye Kata ya Makuburi Prof. Kitila amesema kujengwa kwa barabara hiyo yenye thamani ya Sh. Bilioni 6.7 ni matokeo ya ushawishi uliofanywa ndani ya Bunge ili kuhakikisha wilaya ya Ubungo inafikiwa na mradi wa DMDP.

“Miongoni mwa kazi za Mbunge ni kuishawishi Serikali na kuishauri hivyo nometekeleza wajibu wangu katika ushawishi nikishirikiana na Wabunge wenzangu na kufanikiwa wilaya yetu kuwa miongoni mwa wilaya zitakazonufaika na DMDP na ninyi Makuburi mmepata neema hiyo kwa barabara yenu kuingizwa kwenye mpango huo” amesema Prof. Kitila Mkumbo.

Pamoja na barabara hiyo ya Mchichani – Makoka Prof. Kitila Mkumbo pia amesema wakazi wa Makuburi na Jimbo la Ubungo kwa ujumla watanufaika na ujenzi wa Kingo za Mito ukiwemo mto China na mto Gide ambayo imekuwa ni changamoto ya muda mrefu kwa wananchi kutokana na mafuriko.

“Jambo la mafuriko kimekuwa ni kilio cha muda mrefu kwa wananchi wa Ubungo lakini fedha zitakazotolewa kwaajili ya kujenga Km. 90 za kingo za mito katika Jiji la Dar es Salaam na Sisi Ubungo tumenufaika” amesema Prof. Kitila Mkumbo.

Katika hatua nyingine Prof. Kitila Mkumbo amesema miongoni mwa suluhisho la kudumu la mafuriko linalowagusa wakazi wengi wa Dar es Salaam ni kujengwa kwa Daraja katika eneo la Jangwani ambapo kiasi cha Sh. Bilioni 500 kinatarajia kutumika.

Prof. Kitila Mkumbo amesema kukamilika kwa miradi yote ya DMDP awamu ya pili, kutabadili kwa kiasi kikubwa taswira na Mazingira ya mkoa wa Dar es Salaam.

Mapema kabla ya kuingia kwenye Mkutano huo wa hadhara Prof. Kitila Mkumbo amekutana na wauza kokoto na mchanga katika eneo la EPZA ambao amewaahidi kuwasaidia kupata eneo mbadala la kufanyia biashara zao.