Na Allan Kitwe, TimesMajira Online, Tabora
KAMPUNI ya Mbolea Tanzania (TFC) imewataka wakulima kuanza maandalizi ya msimu mpya wa kilimo mapema huku ikiwahakikisha kuwa mbolea itakayosambazwa ni yenye ubora na viwango sahihi na itawafikia kwa wakati.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa TFC Samwel Mshote alipokuwa akiongea na mwandishi wa gazeti hili jana katika viwanja vya maonesho ya nane nane Ipuli Mkoani hapa.
Amesema kuwa serikali imefanya jitihada kubwa ili kuhakikisha mbolea ya ruzuku itakayosambazwa kwa wakulima msimu huu inakidhi viwango vyote vinavyotakiwa ili kuwezesha wakulima wa Mikoa yote kufanya kilimo chenye tija.
Amefafanua kuwa taratibu zote uagizaji na kuthibitishwa ubora wa pembejeo husika zimeshafanywa na vyombo vya udhibiti ubora nchini, Shirika la Viwango (TBS), hivyo akawatoa hofu wakulima kuhusiana na ubora wa pembejeo msimu huu.
Mshote amebainisha kuwa msimu uliopita waliagiza na kusambaza mbolea katika Mikoa yote kwa wakati vivyo hivyo kwa mwaka huu hawatawaangusha wakulima, watahakikisha mikoa yote 26 inafikishiwa kwa wakati.
‘Tumepita katika Mikoa yote na kufanya tathmini, wakulima wote waliouziwa mbolea wakiwemo wa Mkoa wa Tabora wameridhika na ubora wake, hata msimu huu sina mashaka, wazitumie vizuri ili kuongeza uzalishaji’, amesema.
Amesisitiza kuwa wataendelea kutoa elimu ya matumizi sahihi ya mbolea kwa wakulima wote ili waweze kufanya shughuli zao kwa weledi mkubwa na kwa matokeo chanya.
Mkurugenzi amedokeza kuwa kitengo cha elimu kimeimarishwa zaidi ambapo watapita katika Mikoa,Wilaya, Kata, Vijiji na Vitongoji katika maeneo yote ambako wakulima wapo ili kuwapa elimu hiyo.
Ametoa wito kwa wakulima wote nchini kuendelea kutumia mbolea zinazosambazwa na Kampuni hiyo ya serikali kwa kuwa hazina ujanja ujanja zenye ujazo katika kila mfuko wa kilo hamsini.
Baadhi ya wakulima John Yamungu na Isaka Mhengera kutoka Wilaya ya Uyui wameishukuru serikali ya awamu ya 6 inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha sekta ya kilimo nchini ikiwemo kuwapunguzia bei ya pembejeo.
Aidha wamepongeza juhudi kubwa zinazoendelea kufanywa na Kampuni ya TFC ili kuhakikisha mbolea inayosambazwa inakuwa na ubora uliothibitishwa na Vyombo vya Udhibiti Ubora nchini ili kilimo kiwape manufaa makubwa.
More Stories
Waziri Mkuu: Tumieni matokeo ya tafiti za kisayansi katika utekelezaji wa mipango ya kitaifa
Zaidi ya wananchi 32,000 Vijiji vya Wilaya za Morogoro na Mvomero kuanza kupata mawasiliano
Wafanyabiashara waomba elimu ya namna watakavyorejea soko kuu