November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TARURA yaokoa zaidi ya sh.40 bil ujenzi wa madaraja

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

WAKALA wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) imeokoa kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni 40 katika ujenzi wa madaraja ya zege 275 yaliyojengwa na Mamlaka hiyo kwa kipindi cha miaka saba tangu kuanzishwa kwake.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye banda la TARURA katika maomeaho ya wakulima na wafugaji yanayoendelea jijini Dodoma viwanja vya Nzuguni ,Mratibu wa Teknolojia Mbadala TARURA Makao Makuu Mhansiai Mshauri Fares Ngereja amesema kiasi kilichookolewa kimeenda kufanya kazi nyingine za maendeleo ya wananchi.

Amesema wao wamekuwa wakijenga madaraja au barabara kwa ubora lakini kwa kutumia vifaa vya gharama nafuu.

“Ndio maana utaona hapa katika ujenzi wa madaraja tu tumeokoa kiasi hicho cha fedha ninkwa sababu tumetumia zege ambapo gharama yake ni shilingi bilioni 10,lakini kama tungetumia kokoto na nondo tungetumia zaidi ya shilingi bilioni 50,na madaraja haya yameenea mikoa yote Tanzania Bara.” Amesema Ngeleja

Pia amesema kwa upande wa barabara wanajenga barabara kwa kutumia teknolojia mbalimbali katika mikoa tofauti ambapo pia wanashirikiana na wadau mbalimbali katika ujenzi wa barabara hizo.

“Hivyo basi,katika maonesho haya TARURA ni wahusika wakuu kwani tunawezesha wakulima kutoka shambani na bidhaa zao kupeleka kwenye masoko, na wakati huo huo wakulima kutoa mazao ya vijijini yaani mashambani kuyapeleka katika maghala mbalimbali,

“Kwa hiyo tumekuja kuonesha njia mbalimbali ambazo tunazitumia kuwawezesha hawa wananchi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa barabara na madaraja ambapo hutumia njia nafuu za ujenzi ili kuifungua nchi kwa kipindi kifupi.”amesema Ngeleja

Fundi Sanifu Mkuu Maabara ya TARURA Jacob Manguye amesema ,ili barabara iwe katika ubora unaotakiwa ,inapaswa ianzie maabara ili kupima sampuli zinazotumika katika barabara husika kama vile udongo,lami au kokoto.

“Maabara ya TARURA ilianzishwa kwa ajili ya kusimamia kazi za barabara zinazosimamiwa na TATRURA kutoka vijijini mpaka Mijini,lengo lake ni kusimamia ubora wa barabara za TARURA zinazotekelezwa katika miradi mbalimbali hapa nchini.”amesema

Amesema ,barabara nyingi zinafeli kwa sababu wengi hawaendi kupima ili kupata uhakika kwamba udongo ule wanaotaka kutumia kujenga kwenye barabara kama umekidhi viwango ili magari yatakayopita hapo barabara ihimili uzito wake bila kubonyea au kusambaratika.