Na Mwandishi wetu,Timesmajira
WIZARA ya Madini kupitia Tume ya Madini kwa kushirikiana na kampuni ya Kidee Mining Ltd wanaendelea kutoa elimu kwa wachimbaji wadogo na wa kati wa madini wanaotembelea Banda la Tume ya Madini katika Maonesho ya Nane Nane yanayoendelea kwenye viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma, namna ya kutumia mfumo wa ‘Monorope System Winchi’
Mfumo huo ni wa kutoa udongo kwenye mgodi kwa kutumia vifaa maalum ambavyo vitamuwezesha mchimbaji kutoa tani 10 hadi tani 13 kwa saa moja tofauti na mfumo wa kizamani wa kutumia ndoo na viroba kutoa udongo mgodini.
Akizungumza Mkurugenzi wa Kampuni ya Kidee Mining (T) Limited, Fey Kidee amesema mfumo huo wa zamani mchimbaji anatoa udongo kilo 60 kwa siku na kumuongezea mzigo mkubwa wa kazi tofauti na mfumo huo wa Monorope ambao unarahisisha.
“Tumekubaliana na Tume ya Madini kutoa elimu kwa wachimbaji wadogo na wa kati nchi nzima ili waufahamu huu mfumo wa kisasa uliopo na kuachana na mfumo wa zamani wa kutumia ndoo na viroba,”amesema Kidee.
Aidha, amesema mfumo huo wa kisasa unasaidia kuongeza mapato kwa Serikali na mchimbaji mmoja mmoja ikiwemo kuokoa muda.
“Kutokana na jitihada za Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan alizozifanya kwenye Sekta ya Madini, tumeweza kuinuka wachimbaji kutoka uchimbaji mdogo hadi kufikia uchimbaji wa kati hivyo ni muhimu sisi kama Kidee Mining kuunga mkono juhudi za Rais Samia kwa kutoa elimu kwa wachimbaji wadogo tukishirikiana na Tume ya Madini ili nao wapande kutoka uchimbaji mdogo kuja uchimbaji wa kati,”amesisitiza.
Kidee Mining (T) Limited inayojihusisha na uchimbaji madini na uuzaji na usambazaji wa vifaa vya uchimbaji madini, uchimbaji wa kisasa, ilianzishwa mwaka 2000 ambapo mpango ni kutanua zaidi matawi yake kwa kuongeza migodi na kutengeneza ajira nyingi kwa watanzania.
Mpaka sasa imeshafungua ofisi katika mikoa ya Arusha, Manyara, Mara, Shinyanga na Geita.
More Stories
Tanzania kuwa mwenyeji Mkutano wa Kimataifa matumizi bora ya Nishati
Madiwani Ilala watoa chakula kwa watoto yatima
Waziri Mkuu: Tumieni matokeo ya tafiti za kisayansi katika utekelezaji wa mipango ya kitaifa