Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma
MKUU wa Mkoa wa Dodoma,Rosemary Senyamule amewataka wataalamu wa sekta za mifugo na uvuvi kupeleka na kufundisha teknolojia za sekta hizo vijijini ili kuwapa wafugaji elimu ya kutosha kuhusu ufugaji wa kisasa kwa lengo la kuleta tija.
Akizungumza, leo Agosti 4, 2024 Mkoani Dodoma alipotembelea kwenye Maonesho ya Kilimo ya Kimataifa (Nane Nane) 2024 yanayofanyika Kitaifa mkoani humo, Senyamule amesema wataalamu wahakikishe teknolojia za kisasa zinawafikia wadau wote wa mifugo na uvuvi, hususan maeneo ya vijijini.
“Wataalamu wachukue hatua ya kwenda kwenye makundi ya wafugaji ili kwenda kuwaelimisha kuhusu teknolojia mpya ya ufugaji na kuhakikisha inawafikia” amesema Senyamule.
Aidha,amesema Serikali ya Awamu ya Sita ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, imefanya mapinduzi makubwa sana katika sekta za mifugo na uvuvi kwani ameshuhudia teknolojia mbalimbali na nzuri katika mabanda ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi.
Senyamule amesema sekta binafsi pia zimepokea mabadiliko hayo ya kiteknolojia, hususan upande wa vijana wa Jenga Kesho iliyo Bora (BBT) ambao wanatumia teknolojia hizi kama ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba.
Pia, ametoa wito kwa wadau wote wa mifugo na uvuvi kutumia fursa hii ya maonesho haya ya Nane Nane ili kuweza kujifunza na kupata ufahamu juu ya teknolojia za kisasa za mifugo na uvuvi.
More Stories
Wagombea CHADEMA wakipewa ridhaa,watakuwa wawazi
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili