November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkojo wa sungura unavyoua wadudu wa mimea

Pichani ni wataalam wakionesha dawa ya kuulia wadudu ikiwa imewekwa katika ujazo tofauti

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

MTAALAM wa Maabara kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) Julius Ngumba,amewaasa wananchi kutumia mkojo wa sungura kama dawa ya kunyunyizia kwa ajili ya kuua wadudu katika mimea.

Ngumba ametoa rai hiyo katika maonesho ya wakulima na wafugaji (88) yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.

Amesema watu wengi wamekuwa wakifuga sungura lakini hawaelewi faida ya mnyama huyo .

Kwa mujibu wa Ngumba , ili mkojo ufanye kazi ya kuzuia wadudu,mfugaji anapaswa kuchanganya mkojo wa sungura asilimia 75 na maji asilimia 25.

“Kwa hiyo mbali ya watu kufikiria kinyesi kama mbolea na nyama ,lakini pia katika mkojo wa sungura unapata dawa ya kuua wadudu .”amesema Ngumba

Amesema katika maonesho hayo ya 88 wamekuja kuonesha wafugaji kwamba unaweza kupata dawa hiyo kwenye mkojo wa sungura .

“Kwa hiyo kama mtu ni mkulima na anafuga sungura hatakiwi kuingia gharama za dawa za dukani kwa ajili ya kuulia wadudu,mkojo wa sungura ni dawa ,na uzuri sungura anakojoa mkojo mwingi,

“Wadudu hawapendi mkojo wa sungura kwa hiyo wakisikia harufu yake , wadudu hawawezi kukaa hukimbia.”