September 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Dkt.Samia kuzindua reli ya mwendokasi Dar-Dodoma,Agosti mosi

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

MKUU wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule
amemshukuru Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kuamua uzinduzi rasmi wa Reli ya Mwendokasi(SGR)kufanyika Dodoma.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa leo Julai 30,2024,Mkonze ilipo Stesheni Kuu Dodoma,Senyamule amesema kuwa uzinduzi huo utafanyika Agosti Mosi ,2024 huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Rais Dkt.Samia na kueleza kuwa uwepo wa treni ya mwendo kasi Dodoma utaleta fursa nyingi za kiuchumi na kijamii.

Amezitaja baadhi ya fursa hizo kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa shughuli za biashara kutokana na uwepo wa usafiri rahisi na wa haraka utakaochangia katika kuimarisha biashara na uwekezaji.

“Wafanyabiashara watakuwa na uwezo wa kufikisha bidhaa zao kwa wakati, na miji mingine itakuwa na fursa za biashara na ushirikiano na Dodoma,kuvutia wawekezaji kwa ujumla Reli ya mwendo kasi itafanya Dodoma kuwa kivutio zaidi kwa wawekezaji ambapo hali hii itachangia ukuaji wa viwanda, hoteli na miradi mingine ya kibiashara,”amesema.

Sambamba na fursa hizo Mkuu huyo wa Mkoa wa Dodoma amesema uwepo wa SGR utaongeza ajira mpya katika maeneo mbalimbali ambapo hali hii itasaidia kupunguza ukosefu wa ajira na kuboresha maisha ya mwananchi mmoja mmoja.

Hali kadhalika amesema itasaidia Kuboresha miundombinu ya usafiri kwa kupunguza msongamano wa magari barabarani, kuboresha usalama, na kupunguza muda wa safari, hivyo kupunguza gharama za usafiri ikiwa ni pamoja na Kukuza utalii.

“Reli itavutia watalii kwa urahisi wa kufika Dodoma na maeneo mengine,hii itasaidia kukuza sekta ya utalii na kuongeza mapato kutokana na shughuli za utalii,kuimarika kwa huduma za kijamii,urahisi wa usafiri utawasaidia wananchi kufikia huduma muhimu kama vile afya na elimu kwa urahisi zaidi, hasa katika maeneo ya vijijini pamoja na Uendelezaji wa maeneo mapya, “amefafanua

Senyamule ametumia nafasi hiyo kuwataka Maofisa Usafirishaji(Bodaboda) watakaofanya usafirishaji wa abiria kwenye eneo hilo kufanya kazi kwa uaminifu na kueleza kuwa hali hiyo itawajengea uaminifu kwa wajeta wao na kuwasiaida kujiinua kiuchumi .

“Ni jukumu letu sote kulinda, kudumisha, na kutumia reli hii kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo,mkiwa waaminifu mtafanya kazi yenu iaminike kwa jamii,tuwajulishe wengine kuhusu manufaa ya reli hii , na tuwe na umoja katika kuhakikisha kuwa Dodoma inakuwa mfano wa maendeleo na ustawi, “amesisitiza Mkuu huyo wa Mkoa wa Dodoma