Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe, Dkt. Doto Biteko amewakumbusha Watumishi wa Wizara ya Nishati na Taasisi zake kuiishi Kauli Mbiu ya Sekta ya Nishati ambayo ni Maneno Kidogo Vitendo zaidi ili kuweza kutoa huduma iliyobora kwa wananchi.
Amesema hayo Julai 27 mwaka huu, wakati Watumishi wa Wizara ya Nishati na Taasisi zilizo chini yake waliposhiriki kwenye Bonanza la Nishati ambalo limefanyika Jijini Dodoma likibebwa na Kaulimbiu Shiriki Michezo Imarisha Afya.
“Sekta ya Nishati ni muhimu kwenye ujenzi wa uchumi wa nchi yetu na tufahamu kwamba Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anatutegemea sisi ili kuweza kutoa huduma hii muhimu kwa wananchi, hivyo watumishi tupendane, tushirikiane na kufanya kazi kwa bidi zaidi ili kusukuma mbele gurudumu la Nishati.” Amesema Dkt.Biteko
Kuhusu Bonanza hilo la Nishati, Dkt. Biteko ameeleza kufurahishwa kwake na morali waliyokuwa nayo Watumishi ambao walishiriki kikamilifu katika michezo mbalimbali na kuahidi kuwa huo utakuwa ni utaratibu wa kila mwaka mara baada ya kufanyika kwa Bunge la Bajeti.
Amesema nia ya kufanya Bonanza la Watumishi ni kuhamasishana ili kuweza kutoa huduma bora zaidi kwa watanzania kwa sababu wanaitegema Wizara ya Nishati na Taasisi zake katika kupata huduma hiyo.
Aidha, amewapongeza Watumishi walioshinda michezo mbalimbali katika Bonanza hilo pamoja Viongozi wa Wizara ya Nishati walioratibu Bonanza husika kwa mafanikio.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu , Mhe. Jenista Mhagama ameeleza kufurahishwa na jinsi Bonanza la Nishati lilivyofanikiwa na kusema kuwa huo ni muitikio wa nia ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha Watanzania wanakuwa na afya njema
na kuepukana na magonjwa yasiyoambukiza ambayo dawa yake kubwa ni mazoezi.
Amesema kuwa, michezo inaimarisha afya inajenga umoja, inaleta furaha na kujenga maarifa mapya ya kuwatumikia watanzania hivyo amempongeza Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko kwa kuasisi Bonanza hilo muhimu kwa Watumishi.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amemshukuru Dkt. Biteko kwa kuanzisha Bonanza hilo ambalo amesema linadumisha upendo miongoni mwa Watumishi, umoja, kuwawezesha wafanyakazi kufahamiana zaidi na kuwaimarisha Watumishi.
Amesema kuwa, anaamini Watumishi wamepata motisha ya kazi kupitia bonanza hilo pamoja na hamasa ya kujipanga na kujiimarisha kwa ajili ya michezo inayofuata.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, naye ameipongeza Wizara ya Nishati kwa kufanya Bonanza hilo mkoani Dodoma hali ambayo imezidi kulifaharisha Jiji la Dodoma na kuchagiza uchumi
Ameahidi kuwa, Serikali mkoani Dodoma itaendelea kuwahamasisha wananchi kufanya mazoezi kama ambavyo Viongozi Wakuu wa Nchi wanahimiza ili kuimarisha afya.
Aidha, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amemshukuru Dkt. Biteko kwa wazo lake la Bonanza ambalo limeleta hamasa kubwa kwa watumishi na kuahidi kwamba Bonanza hilo sasalitafanyika kila mwaka.
Amesema Taasisi zote chini ya Wizara Nishati zimeshirki bonanza hilo ikiwemo Kampuni Tanzu za Taasisi hizo.
Kwa nyakati tofauti, Watumishi wa Wizara na Taasisi walioshiriki Bonanza la Nishati wamemshukuru Dkt. Biteko kwa kuanzisha bonanza hilo ambalo wamesema kuwa si tu limechangia kuimarisha afya zao bali pia limewawezesha kufahamiana na watumishi wengine ndani ya Sekta ya Nishati.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko ametunukiwa nishani ya michezo ikiwa ni kutambua mchango wake katika ufanikishaji wa Bonanza la Nishati huku wazo la kuanzishwa kwa bonanza hilo likianzia kwake.
Washindi wa kwanza katika michezo mbalimbali iliyoshindaniwa katika Bonanza hilo ni; Kuvuta Kamba Wanawake (Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania ( TPDC), Kuvuta Kamba Wanaume (TPDC), Volleyball (TANESCO), Mpira wa Pete (TANESCO), Mpira wa Miguu (TANESCO) na mshindi wa jumla ni EWURA.
Baadhi ya Michezo iliyofanyika kwenye Bonanza hilo ni Kupokezana vijiti wanaume, Kupokezana Vijiti Wanawake, Rede, Karata, Riadha, Kukimbia na yai, Kukimbia ndani ya gunia, Kukimbia na maji kwenye glasi, Kupenya ndani ya pipa, Mpira wa miguu, Mpira wa Pete, Bao na
Karata.
More Stories
Mhandisi Samamba awasisitiza maafisa madini kusimamia usalama wa migoni msimu wa mvua
Wapinzani kutimkia CCM ishara ya ushindi Uchaguzi Serikali za Mitaa
Vikundi Ileje vyakabidhiwa mikopo ya asilimia 10, DC Mgomi avipa somo