Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi nchini na Kampuni inayojihusisha na utoaji fedha katika kuendeleza sekta ya ujenzi nchini Korea Kusini (K-FINCO), zimetia saini mkataba wa ushirikiano baina ya pande mbili hizo, katika hafla iliyofanyika Makao Makuu ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Jijini Dar es Salaam.
Katika hafla hiyo iliyoshuhudiwa na Balozi wa Tanzania nchini Korea Kusini Bw. Togolani Mavura, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhandisi Anthony Sanga, alitia saini makubaliano hayo kwa niaba ya Serikali ya Tanzania, wakati Afisa Mtendaji Mkuu wa K- FINCO, Bi. Lee Eun Jae, alitia saini makubalino hayo kwa niaba ya Serikali ya Korea Kusini.
Shirika la Kifedha za Ujenzi la Korea (K-FINCO), ni Shirika la Serikali lililopo chini ya usimamizi wa Wizara ya Ardhi, Miundombinu na Uchukuzi ya Korea Kusini (MoLIT), imekuja nchini Tanzania ili kutafuta fursa za uwekezaji wa kukuza maendeleo ya sekta ya ujenzi nchini.
Shirika hilo linatoa huduma mbalimbali za dhamana na bima kulingana na mahitaji ya makampuni ya ujenzi, kusaidia ukuaji wao na uhimilivu. Hii husaidia kuhakikisha sekta ya ujenzi inakuwa imara kwa kupunguza hatari za kifedha na kukuza mazoea endelevu ya biashara miongoni mwa wanachama wake.
Akizungumza katika hafla hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhandisi Anthony Sanga, alisema kuwa kampuni hiyo ya Korea Kusini, imekuja nchini Tanzania kuangalia fursa za uwekezaji katika makazi nchini kufuatia mwaliko wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, alioutoa kwa wawekezaji mbalimbali wa nchi hiyo kuja kuwekeza Tanzania, alipofanya ziara yake nchini Korea Juni, 2024.
“Kuja kwa kampuni ya (K-FINCO), hapa nchini, kunafungua milango ya uwekezaji kutoka nchini Korea Kusini, ya ujenzi wa nyumba, lengo kuu likiwa ni kupunguza ombwe la makazi nchini. Mkataba ambao umesainiwa leo, kama nilivyosema awali, unalenga pande mbili hizo kushirikiana katika kupambana na upungufu wa nyumba nchini kama ilivyobainika katika sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, iliyobainisha kuwa kuna upungufu wa nyumba milioni tatu, “amefafanua Mhandisi Sanga.
Mhandisi Sanga, amesema kwa mujibu wa matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, ni bayana kuwa taasisi za ndani ya nchi zikiwemo Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Wakala wa majengo Tanzania (TBA), Watumishi Housing na kampuni ya mikopo ya nyumba (TMRC), inayowezesha taasisi za fedha kutoa mikopo ya muda mrefu kwa wananchi wanaonunua nyumba, haziwezi kumaliza ombwe la nyumba za gharama nafuu.
“Wenzetu wameendelea katika masuala ya ujenzi kufuatia teknojia ya kisasa ya ujenzi waliyo nayo hivyo ushirikiano na (K-FINCO), natumaini utakuwa na matokeo chanya ikiwemo kubadilishana uzoefu wa ujenzi wa nyumba hususan za gharama nafuu, kupunguza gharama za ujenzi na kutoa fursa za ajira wakati wa utekelezaji wa miradi husika, ” alikazia Sanga.
Katika hatua nyingine Mkurugenzi wa Uendelezaji Biashara wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Bw. William Genya, alitoa wasilisho mbele ya ujumbe huo kutoka nchini Korea, ambapo aliainisha maeneo mbalimbali ya NHC ambayo (K-FINCO), inaweza kushirkiana katika kuongeza kasi ya ujenzi wa nyumba.
Bw.Genya, ameyataja maeneo ambayo K- FINCO, inayoweza kushirikiana na NHC kuwa ni pamoja na maeneo yaliyopo katikati ya miji na majiji nchini, ikiwemo Dar es Salaam na Arusha, ambapo NHC ina ardhi kubwa inayohitaji uwekezaji wa nyumba za makazi na biashara. Aliyataja maeneo mengine kuwa ni eneo la Kawe Tanganyika Packers, Usa River Arusha, Salama Creek Jijini Dar es Salaam na mradi wa Samia Housing Scheme ambao unakusudia kujengwa nyumba 5000 katika maeneo mbalimbali nchini.
Ujumbe huo wa K-FINCO, Julai 27, 2024 unatarajiwa kutembelea miradi ya NHC ya Jijini Dar es Salam ikiwemo mradi wa nyumba za makazi wa KAWE 711, Samia Housing Scheme Kawe, Morocco Square na eneo la Upanga linalotarajiwa kuendelezwa upya.
More Stories
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa
NLD kipo tayari kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa