September 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ulenge:Nitaendelea kuwapigania wanawake wajikomboe kiuchumi

Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Handeni

MBUNGE wa Viti Maalumu Mkoa wa Tanga Mhandisi Mwanaisha Ulenge amesema dhamira yake ni ya dhati katika kuwakomboa wanawake wa mkoa huo kiuchumi, kwani nia yake ni kuona mwanamke anasaidiwa na kile alichoshika mkononi kwa kukitafuta kwa nguvu zake.

Amedai kama atatokea mtu wa kumpinga yeye, basi huyo anapinga maendeleo ya wanawake wa Tanga ikiwemo jitihada anazofanya kama kuwatafutia na kuwapa wanawake mbegu za mazao mbalimbali kwa ajili ya kujikita kwenye kilimo.

Ameyasema hayo Julai 19, 2024 wakati anazungumza kwenye Baraza la Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Wilaya ya Handeni lililofanyika Ukumbi wa CCM mjini Handeni na kuongeza kuwa mbegu za mazao mbalimbali alizowaletea ikiwemo alizeti ni kwa ajili ya wao kuweza kujitegemea kiuchumi.

Mhandisi Ulenge amesema haiwezekani kuona Mkoa wa Tanga ukiwa na ardhi yenye rutuba, lakini wanawake wameshindwa kulima zao la alizeti na kuajiri vijana wao na kupanga vidonga (vidumu) vya mafuta kwenye barabara kuu ya kutoka Dar es Salaam kwenda Arusha kama ilivyo wanawake wa Mkoa wa Singida.

“Malengo yangu ni malengo yenu na nataka kuwaambieni wenzangu hii yote ni vita ya kiuchumi kwa wanawake wa Mkoa wa Tanga mniombee, mkisikia Ulenge anapigwa vita mjue yanapigwa vita maendeleo yenu, mniombee, shetani hawezi kufurahia kuona mnapata mkombozi wa kweli” amesema Mhandisi Ulenge.

Mhandisi Ulenge amesema hata Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kilimo amekipa kipaumbele na amepeleka nyenzo nyingi kwa maofisa ugani ikiwemo pikipiki na kompyuta ili kuona wanawatumikia wakulima hivyo wakulima hasa wanawake wanatakiwa kuwafuata maofisa ugani hao na kuwaeleza waende kwenye mashamba yao na kuwapa utaalamu ili walime, kupanda na kuvuna kwa tija.

Mhandisi Ulenge amesema, pamoja na changamoto mbalimbali zinazowapata wakulima,bado anaamini dhamira na malengo yake bado yapo pale pale na atapambana kuona anapata mbegu bora.

“Tuwashike mashati maofisa ugani wetu ili waweze kutuongoza vizuri,wako hapo kwa ajili ya Mama Samia na Mama Samia amewapa vitendea kazi ikiwemo laptop (kompyuta) na pikipiki ili waweze kutusaidia sisi wakulima na agenda yangu ya kilimo bungeni sitaacha sababu Tanga ardhi yetu ni nzuri.

“Utaona wenzetu wa mikoa ya jirani wanakimbilia Handeni wanachukua maeneo wanalima, sisi kwa nini turudi nyuma, nataka tulime kilimo chenye tija na ndiyo maana natafuta mbegu bora ili tulime kilimo chenye tija na kisambae maeneo mengi na kupata mazao yenye tija zaidi. Hivyo agenda yangu ile naomba muipokee” amesema Mhandisi Ulenge.

Mhandisi Ulenge amesema kama kilimo kitapewa mkazo, hakutakuwa na upungufu wa chakula hata kwa wanafunzi wanaosoma shuleni, kwani watakuwa na uhakika wa kula mchana wakiwa shuleni, lakini pia suala la udumavu kwa watoto halitakuwepo.

Akifungua baraza hilo, Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Handeni Sophia Masimba amesema Mhandisi Ulenge ameonesha nia ya dhati ya kuwasaidia kuwakwamua kiuchumi wanawake wa Mkoa wa Tanga, kwani amekuwa akibuni mbinu mbalimbali za kuwatoa kwenye umasikini kwa kuwapa mbegu za mazao mbalimbali ili waweze kutoka kimaisha na kuondoa utegemezi.

Naye Katibu wa CCM Wilaya ya Handeni Mayasa Kimbau amemuelezea Mhandisi Ulenge kama Mbunge mwenye shukrani kwa kuwatakia mema wanawake wa Mkoa wa Tanga wa kuwatoa kwenye umasikini na kuona wanasimama imara kiuchumi, kwani mtu anaekutakia mema hawezi kukupa samaki bali anakupa nyavu ili upate samaki wengi.