September 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mzee miaka 63, auawa kikatili,alichukuliwa na watu wasiojulikana usiku wa manane

Na Moses Ng’wat, Mbozi.

KUMINYA Sambo (63), Mkazi wa kijiji cha Nambizo, wilaya ya Mbozi, Mkoani Songwe, amekutwa akiwa amekufa baada ya kuuawa na watu wasiojulikana kisha mwili wake kutupwa katika moja ya msitu kijijini hapo.

Taarifa zilizothibitishwa na ndugu pamoja na uongozi wa kijiji zinaeleza kuwa marehemu ambaye alikuwa akiishi bila mke alitoweka nyumbani kwake siku kadhaa kabla ya kukutwa akiwa ameuawa, huku viungo vya mwili wake ikiwepo mguu na mkono vikiwa vimenyofolewa.Mmoja wa watoto wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Jose Kuminya Sambo, amesema baba yao alikutwa ameuwawa baada ya kupotea kwa takribani siku tatu .

Jose amesema Mzee Sambo alipotea nyumbani nyakati za usiku Julai 9, 2024 na kwamba kitihada za kumtafuta kwa kushirikiana na wananchi ziliendelea kwa siku tatu bila mafanikio hadi ilipofika Julai 11,2024 pale walipomkuta akiwa ameuawa na mwili wake kutelekezwa kando ya njia katika moja ya msitu kijijini hapo, huku mguu mmoja na mkono vikiwa vimenyofolewa.

Ameongeza kuwa, kuwa mazingira yaliyokutwa nyumbani kwa baba yao ambaye alikuwa akiishi peke yake siku aliyotoweka yalizua hofu kubwa kwani walikukuta hakuna dalili zilizoonyesha kama nyumba ilivunjwa.

“Lakini cha kushangaza kwa kuwa mlango haukuvunjwa hali inayoonesha watu waliomchukua baba (marehemu) na kwenda kumuua waliondoka naye baada ya kumgongea na yeye kuwafungulia mlango kwani hata pombe aliyokuwa akitumia usuku ule ilikutwa kwenye kopo ikiwa pembeni” amesimulia kwa hisia kali mtoto huyo wa marehemu unya uchunguzi.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Namanga kijijini hapo, Jackson Ntembo, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa, baada ya kupewa taarifa za kupotea kwa Mzee Sambo tulianza kumtafuta na hatimaye kumkuta akiwa amefariki huku akiwa amekatwa mapanga kifuani, kichwani huku mguu mmoja na mkono vikiwa vimeondolewa.

“Daktari aliufanyia uchunguzi mwili wa marehemu na kukuta una majeraha manne ambayo yalisababishwa na kukatwa na kitu chenye nchakali, na Mimi kama kiongozi naliomba jeshi la polisi kufanya uchunguzi zaidi juu ya tukio hilo,” amesema Ntembo. Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Gallus Hyera amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba wanaendelea na uchunguzi na kubainisha kuwa hakuna mtutu yeyote aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo.

Wilaya ya Mbozi imekumbwa na matukio ya mauaji ikikumbukwa kuwa hivi karibuni watu wasiojulikana walimua aliyekuwa Mfamasia wa Kituo cha Afya cha Isansa, Wilayani hapa, Daudi Kwibuja (30) na mwili wake kukutwa kando ya barabara Kuu itokayo Mbeya kwenda Tunduma (Tanzam) katika eneo la Mlowo, Wilayani hapa.

Mwili wa mtumishi huyo ulikutwa ukiwa na majereha mwilini mwake na kwenye taarifa yake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Agostino Senga, ambaye kwa sasa yuko likizo alisema kuwa uchunguzi ulionesha kuwa majeraha yaliyokutwa kwenye mwili wa marehemu hayakufana na majereha ya ajali ya kugongwa na gari licha ya awali kudhaniwa kuwa marehemu alifariki kwa ajali ya kugongwa na gari.

Pia katika tukio hilo hadi kufikia sasa hakuna mtu yeyote aliyekamatwa na jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi.