November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mhandisi Mahundi awataka wanawake kujitokeza kugombea nafasi za uongozi

Na Esther Macha, Timesmajira Online, Mbeya

WANAWAKE Mkoa wa Mbeya wametakiwa kuwa chachu ya kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu ili kuondoa mashaka kwa lengo la kujiimarisha katika nafasi mbalimbali za uongozi.

Kauli hiyo imetolewa na Mbunge viti maalum Mkoa wa Mbeya ambaye pia ni Naibu Waziri wa habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Maryprisca Mahundi wakati wa mkutano wa mkuu wa Baraza la UWT Wilaya ya Mbeya.

Mhandisi Mahundi amesema kuwa ni wakati sasa kwa wanawake kujitokeza kwa wingi kutia nia katika kugombea nafasi za uongozi.

“Tunaelekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu ndugu zangu wanawake wote wa mkoa Mbeya chukueni fomu za kugombea katika nyanja mbalimbali za uongozi najua mpo wenye uwezo wa kuongoza hivyo ni vyema kutumia nafasi hii ya uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu”amesema Mhandisi Mahundi.

Hata hivyo Katika ziara hiyo , Mhandisi Mahundi amewataka Wanawake kuwa na miradi itakayowawezesha kujikwamua kiuchumi.

Amesema kuwa kila mwanamke ana wajibu wa kuhakikisha kuwa anakuwa shughuli ya kufanya ya kumwingizia kipato chake ili aweze kuendelea maisha yake pasipo kuwa tegemezi.

Hata hivyo Mhandisi Mahundi ambaye pia ni Mbunge wa vitimaalum mkoa wa Mbeya amesema kuwa hatakuwa tayari kuona ufujaji wa pesa zilitolewa kwa ajili ya umoja wa wanawake ( UWT)

Akiahirisha Kikao cha Baraza Mwenyekiti wa UWT Wilaya Mbeya Subira Mwangoka amewataka wanawake kuendelea kuwa na mshikamano wa moja na kuepukana na chuki ambazo zinaweza kusambaratisha mshikamano.

Ziara ya Mbunge wa Viti Maalum imeanzia Wilaya ya Chunya lengo ni kuimarisha jumuiya,kuimarisha uchumi na kuhimiza ushiriki wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu.