October 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watumishi wa Umma wawezeshwa mikopo ya zaidi ya Bil. 100

Na Allan Kitwe, TimesMajira Online, Tabora

CHAMA cha Ushirika wa Akiba na Mikopo cha HAZINA SACCOS Ltd kimewezesha wanachama wake (watumishi wa umma) kupata mikopo ya zaidi ya sh bil 100 tangu kuanzishwa kwake.

Hayo yamebainishwa leo na Mtendaji Mkuu wa Taasisi hiyo Festo Mwaipaja alipokuwa akizungumza na wanahabari kwenye Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani (SUD) yanayofanyika Kitaifa Mjini Tabora.

Amesema kuwa mfuko huo ulioanzishwa mwaka 1972 na kusajiliwa mwaka 1973 ulilenga kuhudumia watumishi wa Wizara ya Fedha pekee lakini baadaye ukahusisha watumishi wa Wizara zote Tanzania Bara.

Amebainisha kuwa chama hicho kilianza na wanachama 250 lakini kutokana na huduma yake nzuri na manufaa makubwa wanayopata wanachama wake hadi sasa kimefikisha wanachama 8,000.

Mwaipaja ameongea kuwa hadi sasa chama kina akiba za wanachama za kiasi cha sh bil 29 ambazo zimetokana na michango yao na wanachama wote wameendelea kunufaika na mikopo minono ya kimaendeleo.

‘Mfuko huu ni mkombozi kwa watumishi wa umma wote Tanzania Bara kwa kuwa wanaruhusiwa kuchukua kiasi chochote wanachotaka wakati wowote kwa utaratibu uliowekwa na kurejesha pasipo usumbufu wowote, hadi sasa tumeshatoa mikopo ya zaidi ya sh bil 100’, ameeleza.

Amefafanua kuwa wana mikopo isiyoangalia akiba, inayoangalia akiba na ya ununuzi wa viwanja, na kupitia mikopo hiyo wanachama wao wameendelea kupiga hatua kubwa kimaendeleo.

Mikopo isiyoangalia akiba amesema kuwa ni ile ya kijamii ambayo ni dharura, elimu, mazishi na sikukuu ambapo mwanachama anaweza kuchukua kati ya sh laki 5 hadi mil 5 kulingana na hitaji lake.

Na mikopo inayoangalia akiba amesema kuwa ni ile ya maendeleo, biashara, ujenzi na hitaji maalumu (standing order) ambapo kiasi kinachotolewa ni kati ya sh mil 20 hadi 50.

Mtendaji Mkuu ameeleza malengo makuu ya taasisi hiyo kuwa ni kuinua maisha ya watumishi wa umma na kuwawezesha kutatua changamoto yoyote ya kimaisha itakayotokea mbele yake ili kukidhi ppmahitaji yao.

Ameongeza kuwa mfuko huo unahudumia watumishi wa umma wa aina zote wakiwemo Viongozi Wakubwa, hivyo akabainisha kuwa wako makini sana katika usimamizi wake, hakuna ubabaishaji wa aina yoyote.