October 7, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Utafiti usalama wa vijana mtandaoni wazinduliwa Dar

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

SHIRIKA la Mulika linalojishughulisha na masuala ya vijana, limezindua ripoti ya utafiti wa ulinzi na usalama mitandaoni kwa vijana katika matumizi ya mitandao.

Akizungumza mara baada ya Uzinduzi wa utafiti huo jijini Dar es salaam ulioenda sambamba na
mdahalo wa vijana na matumizi ya mitandao, Ofisa Uchechemuzi na Mawasiliano wa shirika hilo, Whitney Satory , amesema asilimia 80 ya vijana waliohojiwa katika utafiti huo wamesema hawapo salama huku asilimia 20 tu wako salama.

Amesema jambo hilo linaonesha uwepo wa pengo kubwa katika kuhakikisha mazingira salama ya mtandaoni kwa vijana nchini Tanzania.

Satory amesema katika maoni yao, vijana wamesema wamekuwa wakitishwa na kudhalilishwa katika utumiaji wa mitandao jambo ambalo huwafanya vijana wengine kuogopa kuitumia.

“Wakati vijana wakisema hivyo, vijana wa kike wamesema wao ndio waathirika wakubwa kwa kuwa picha zao za utupu zimekuwa zikisambazwa na nyingine wakiwa faragha ,”amesema Satory

Amesema malengo ya utafiti huo imetokana na kuwepo ongezeko la vijana wanaotumia mitandao na kutaka kujua usalama wao, vikwazo wanavyopitia na kupeleka maoni hayo kwa mamlaka ili kujua namna gani wanazifanyia kazi.

“Utafiti ulikusanya majibu kutoka kwa vijana 160 kupitia mtandao, ukilenga rika mbalimbali na maeneo ya kijiografia kote Tanzania.

“Matokeo ya utafiti yalionesha kuwa wengi wa waliohojiwa walikuwa wanawake asilimia 58 kati ya umri wa miaka 20-24 (40,%) na 25-29 (28,%). Utafiti ulionesha kuwa asilimia 84 ya waliohojiwa walitoka maeneo ya mjini, jambo linaloonyesha kuwepo kwa pengo la upatikanaji wa mtandao kati ya vijana wa vijijini na mijini,”amesema.

Katika maoni yao vijana akiwemo Michael Ndaki wametaka elimu zaidi itolewe ya namna ya kuwaripoti wanaowadhalilisha na wale wanaowatisha kwa kuwa wengi wameishia kupata msongo wa mawazo kwa kutojua nini cha kafanya wanapofikwa na hali hilo.

Awali akizungumza katika mdahalo huo, Ofisa Tehama Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania(TCRA), Irene Kahwili, amewataka vijana wanaodhalilishwa mitandaoni kuripoti polisi ili hatua zaidi ziweze kuchukiliwa.

“Kumekuwepo na tabia za watu kuja kuripoti TCRA pale wanapodhalilishwa mitandaoni, naomba niwambie hilo ni kosa kama makosa memgine ambayo yanapaswa kuripotiwa polisi,”amesema.

Kwa upande wake Mkaguzi Msaidizi wa Polisi kutoka kitengo cha makosa ya kimtandao, Alpha Assey, amewashauri vijana kuchagua lugha na vitu vya kuandika mitandaoni ili wasije wakajikuta wanaingia matatizoni.

“Hapa naomba nisisitize si kila kinachopostiwa mtandaoni si lazima utoe maoni yako unaweza ukachambua kwamba unafaa kulitolea maoni au la na kwa lugha gani ili baadaye usije ukajikuta unaingia matatizoni kwani hakuna utoaji maoni usiokuwa na mipaka,”alisema Assey.

Licha ya kuwepo kwa changamoto lakini vijana pia walikiri kuwepo kwa fursa katika mitandao ya kijamii.

Wamesema changamoto bado ipo katika bei za vifurushi na uimara wa upatikanaji wa mtandao.

Marry Mbago amesema hali hiyo inaweza kuwakosesha fursa hizo vijana wengi hasa waliopo vijijini ambao vipato vyao ni vya chini si kwao tu bali hata kwa wazazi na walezi wanaowategemea.