December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

UVCCM Ileje wahamasishana uchaguzi serikali za mtaa

Na Moses Ng’wat, Ileje.

UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (Uvccm) Wilaya ya Ileje, Mkoani Songwe, wametakiwa kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi za uongozi katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu 2024.

Hamasa hiyo imetolewa Juni 19,2024 na Mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Diana Ngambo, wakati wa kikao cha baraza la kikanuni cha umoja huo kilichofanyika katika Ukumbi wa chama hicho uliopo mjini Itumba wilayani humo.

Ngabo amesema ni wakati wa vijana kujitokeza kugombea nafasi za uongozi kwa lengo la kupata watu watakaoendana na kasi ya kusimamia miradi ya maendeleo.

“Tunataka vijana ndio washike nafasi za uongozi na wazee wetu wabaki kuwa washauri ili tukikosea waturekebishe, hivyo vijana wenzangu tujitokeze kuomba nafasi muda wa uchukuaji fomu utakapotangazwa na tume ya uchaguzi,” amehimiza Ngabo.

Kwa upande wake Katibu wa Jumuiya hiyo Wilaya, Fatma Mohamed, amewasisitiza vijana hao kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kwenda kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura ili wawe na sifa ya kupiga kura wakati wa uchaguzi.

“Sifa moja wapo ya kuwa mpigakura lazima uwe umejiandikisha kwenye daftrai la kudumu ambapo zoezi lake linatarajia kufanyika hivi karibu hivyo mijiandikishe na muwe mabalozi wema kwa wananchi ili wajitokeze,” amesema Fatuma.

David Mbughi, Katibu wa Vijana Kata ya Luswisi amesema wanatakiwa kutoogopa kushiriki uchaguzi kwa vitisho kwani wananafasi ya kuwa viongozi bora na wenye nia ya kuleta maendeleo.

Naye, Mjumbe wa Baraza la Uvccm Wilayani humo, Adamu Myala, amesema kama vijana wapo tayari kugombea nafasi za uongozi kwenye uchaguzi ujao kwani vijana wanambio na wazee wabaki washauri.