September 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TLS:Wananchi bado wanahitaji Katiba mpya

Na Mwandishi wetu, Timesmajira

Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kimesema kuwa wananchi bado wanahitaji Katiba Mpya ambayo ni mustakabari wa maendeleo nchini.

Akizungumza wakati akifungua mjadala kwa wanafunzi wa vyuo vikuu mbalimbali nchini juu ya ‘Mchakato wa Upatikanaji wa Katiba Mpya,Mkurugenzi wa Mtendaji wa TLS, Mariam Othuman amesema wameamua kuandaa mjadala huo kwa kundi la vijana ni muhimu.

Amesema mijadala kama hiyo wamekuwa wakifanya kwa makundi mbalimbali”Kwa kuangalia majukumu tuliyonayo pamoja na Mchakato wa Katiba unaoendelea tukaona kuna umuhimu wa kuanzia mijadala mbalimbali ya kuongelea masuala ya mchakato wa Katiba Mpya,”amesema na kuongeza

“Tukaona ni vyema kupitia kundi hili ambalo ni Maalum na ni kundi mojawapo, tukiangalia sensa ya mwaka 2022 inasema asilimia 34.5 ya Watanzania ni vijana. Kwahiyo tukaona hili ni kundi muhimu sana kuwasikiliza na kupokea maoni yenu juu ya mchakato wa Katiba Mpya. Hivyo tunaamini mtatoa maoni yenu kwasababu nyie ndo chachu ya maendeleo katika Taifa. Tunawatia moyo yote ambayo tutajadili hapa tutayachukua na kuyafanyia kazi ili tuweze kuyafikisha katika mamlaka husika,” amesema Mariam.

Kwa Upande wake Afisa Miradi TLS, Victor Mbuligwe amesema Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 ina mapungufu na ndio maana ulianzishwa mchakato wa kupata Katiba Mpya ambao mwaka 2014 ulikwama.

“Tunaona serikali ina nia ya dhati kuufufua huo mchakato kwahiyo sisi tumeamua kuanza kuyakusanya haya Makundi tofauti ili kupata maoni yao kitu gani ambacho wanafikiri kiwepo kwenye hiyo katika mpya wanayoitarajia.

“Hivyo bado sisi tunahitaji Katiba Mpya na inahitajika na wananchi na kwa kauli ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliwahi kusema wananchi wanahitaji Katiba yao,” amesema Mbuligwe.

Naye Thomas Alfred ambaye ni wanafunzi wa Chuo cha Sheria amesema amesema mijadala hiyo ni muhimu kwa wakati huu ambao kilio kikubwa ni kupatikana kwa Katiba Mpya.