September 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wazee walalamikia ukatili na unyanyasi kwa familia

Na Esther Macha, TimesMajira Online, Bunda

VITENDO vya ukatili na unyanyasi ambavyo vimekuwa vikiendelea kufanywa na vijana, jamii katika mkoa wa Mara vimewaibua wazee na kulaani tabia hiyo na kuomba serikali kutunga sheria ya kuwalinda na kuwatambua .

Hayo yamesemwa Juni 14,2024 wakati wa kongamano la kimataifa la siku ya kupinga ukatili dhidi ya wazee Juni 14,2024 katika Chuo cha Ualimu Bunda mkoani Mara.

Debora Saru kutoka mkoa wa Mara amesema kuwa kumekuwa na matukio mengi ya wazee kufanyiwa ukatili na vijana au watoto wao hali ambayo inaumiza wazee walio wengi na kushindwa kusema matukio hayo .

“Wazee wanawake wamekuwa wakiingiliwa kinguvu kimapenzi na vijana na baadhi yao kulawiti tunaomba vyombo vya sheria kutusaidia katika hili wengi wanafanyiwa hivi vitendo ila kuongea hawezi matukio mengi yanaishia kwenye familia kutungwa kwa Sheria ndo kutakuwa tiba kwetu”amesema Mzee huyo

Ferister Nyambala ni mkazi wa wilaya ya Tarime amesema kuwa matukio ya mauaji ya wazee hayafuatiliwi kutokana na vyombo vya sheria kutofuatilia na kuwa pia ili malalamiko dhidi ya wazee yasiendelee kuwepo itungwe sheria ambayo itawatambua wazee pamoja.

“Mzee anaenda kulalamika kwenye vyombo vya sheria lakini jambo lake halichukuliwi uzito na hata hizi halmashauri za wilaya bado zimekuwa ngumu kututambua hivyo tunaomba pia nazo zitunge sheria kutambua haki za wazee ,ndo maana sasa unakuta vitendo vya ukatili kwa wazee vinazidi kuendelea katika jamii pasipo shaka “amesema Mzee Nyambala.

Akizungumza wakati wa mjadala wa kongamano hilo ,Mkuu wa wilaya ya Bunda mkoani Mara Dkt .Vicent Aney amesema kuwa kwa mkoa wa Mara kumekuwa na vipigo vya wazee kutoka kwa watoto wao ,kuingiliwa kinguvu kimapenzi,kunyima chakula,kunyimwa urithi.

“Hivi karibuni kuna kuna rafiki yangu kutoka nje ya mkoa huu alinipigia simu akilalamikia ndugu yake kuwapiga wazee wake hali iliyolazimu wazee hao kujifungia ndani kwa kukwepa mauaji ,ilibidi nitumie polisi kumsaka kijana huyu , changamoto kubwa ni mtazamo hasi juu ya uzee na kuzeeka “amesema Dkt.Aney.

Akielezea zaidi mkuu huyo wa wilaya amesema kuwa wazee walio wengi wametelekezewa kulea wajukuu na watoto wao pasipo msaada wowote hali inayowalazimu wazee kuwatuma kuomba fedha mitaani ili waweze kujikimu kimaisha.

“Hawa watoto wengi wao hawaendi shule kutokana na muda mwingi kutumia kuomba fedha ambazo hutumwa na bibi zao ambapo hutumia muda mwingi kuzunguka mtaani kuomba fedha ambayo huwawezesha kuishi “amesema Dkt.Aney.

Joseph Mbasha ni mkuu wa Kitengo kutoka Shirika lisilokuwa la kiserikali linalojishughulisha na masuala ya wazee HelpAge Tanzania amesema kuwa kwa ukanda wa mkoa wa Mara kumekuwa na matukio ya wazee kupigwa na kunyanyaswa na watoto .

Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo ni Waziri wa maendeleo ya Jamii jinsia, wanawake na makundi maalum Dkt.Doroth Gwajima na Kauli mbiu ya mwaka huu ni Utu, Usalama na ustawi ni Nyenzo ya kutokomeza ukatili dhidi ya wazee .

Baadhi ya wazee na vijana walioshiriki kongamano hilo kutoka mkoa wa Mara,Wilaya ya Bunda, Musoma,Geita,Tabora
Mkuu wa wilaya ya Bunda Dkt.Vicent Aney (wa tatu kushoto)
Joseph Mbasha mkuu wa Kitengo kutoka Shirika lisilo kuwa la kiserikali linalojishughulisha na wazee HelpAge Tanzania