January 9, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Agizo la Samia Treni Reli ya SGR latimia, kuanza rasmi safari kesho

*Kuanza safari zake kuanzia kuanzia kesho kwenda Morogoro, ni usafiri wa kwanza wa kiwango hicho kuanza kutumika hapa nchini

Na Na Jackline Martin,Timesmajiraonline

SIKU iliyokuwa ikisubiriwa kwa miaka mingi tangu Tanzania ipate uhuru imewadia, baada ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, kupitia Shirika la Reli Tanzania (TRC) kutangaza kuanza usafari wa Treni ya Reli ya Kisasa (SGR) kuanzia Juni 14, mwaka huu (Ijumaa).

Kuanza kwa safari hizo ni utekelezaji wa agizo la Rais Samia la kutaka TRC ifikapo Julai, mwaka huu treni hiyo iwe imeanza kutoa huduma..

Kuanza kwa safari za treni hiyo kumetangazwa jana Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa TRC, Masanja Kadogosa, wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye hafla ya uzinduzi wa kampeni ya uelewa kuhusu kuanza kwa huduma za usafiri wa treni hiyo yenye kaulimbiu isemayo; “Twende tukapande Treni yetu, tuitunze, tuithamini’.

Alisema kuanza kwa safari hiyo Juni itapelekea kugundua changamoto mapema za kwenye reli hiyo na kuweza kuzitatua kwa wakati.

“Shirika litaanza kutoa huduma za awali za usafiri wa treni katika Reli ya kiwango cha kimataifa SGR kwa Dar es Salaam – Morogoro ifikapo Juni 14, 2024.

Kuanza kwa safari za treni Dar es Salaam – Morogoro ni sehemu ya kuendelea kujifunza kwa kuwa teknolojia hiyo mpya nchini na kujiridhisha kwa mifumo mbalimbali ya uendeshaji huduma za usafiri wa treni kabla ya kuanza rasmi safari ya kutoka Dar es Salaam Dodoma ifikapo Juali 25, 2024,” alisema Kadogosa.

Pia aliwataka wanachi waendelee kushirikiana kutunza miundombinu ya Reli hiyo kwani ni Mali ya watanzania na imejengwa kwa fedha za walipakodi wa Tanzania kwa kutumia huduma za TRC ili kuongeza pato la Taifa.

Aidha alisema ndani ya Reli hiyo kutakua na ulinzi wa kutosha kwa reli yenyewe, abiria na mizigo kwa ujumla.

“Jambo hili ni muhimu sana kwa maana ya usalama wa reli yetu, usalama wa abiria na mizigo, kwani ukiacha kuwa na CCTV Camera tutakua na watu ambao watakuwa wanaangalia kile kinachoendelea kwenye treni yetu kwa masaa 24, pia uwepo wa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama ambapo tutakua na askari kwenye treni ambao watasafiri nasi mwanzo hadi mwisho”

“Kwenye miundombinu, pamoja na kufanya doria, stesheni zetu zote zina vituo vya polisi na tuna imani kuwa kutakua na utaratibu wa kuwepo na askari huko njiani, pia Askari watafanya doria, tutakua na walinzi watakuwa wanafanya kazi masaa 24”

Kadhalika Kadogosa alisema abiria wanaweza kukata tiketi kwa njia ya mtandao au kupitia madirisha ya kukatia tiketi ndani ya stesheni ambapo kupitia njia ya mtandao abiria atatakiwa kukata tiketi wiki moja au siku tatu kabla ya safari ili kuepukana na msongamano.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Biashara (TCB) Adam Mihayo, alisema katika safari hizo za Reli ya SGR, TCB wameshirikiana na TRC kukusanya mapato katika vituo vya kukatia tiketi.

Pia Mihayo alisema Benki ya TCB wameshirikiana na TRC kwa kufanikisha kuleta vichwa vya treni na mabehewa kutoka Ujerumani.

“Ushirikiano wetu na Reli ya Tanzania unaakisi dhamira yetu ya pamoja ya kuelewa mahitaji ya Watanzania na kuchangia katika ukuaji wa maendeleo ya kiuchumi na mafanikio ya Taifa letu,” alisema

“TCB tutaendelea kushirikiana na shirika la Reli Tanzania ili kuhakikisha matarajio ya Rais katika mradi huu yanaweza kutimia,” alisisitiza.

Kwa mujibu wa viwango vya nauli za treni ya SGR vilivyotangazwa na LATRA juzi, nauli ya mtu mzima kutoka Dar es Salaam kwenye Dodoma itakuwa sh. 31,000.

Kwa upande wa watoto kuanzia miaka 12 kushuka chini watakuwa wakilipa nusu ya gharama.

Nauli hiyo inapishana kwa kiasi kidogo na nauli ya mabasi kwa ruti hiyo, ambapo nauli ya Dar es Salaam kwenda Dodoma, inaanzia sh. 29,000 hadi sh. 35,000 kulingana na aina ya daraja.

Aidha nauli kutoka Dodoma hadi Makutupora kwa mtu mzima atalipa sh. 37,000 na watoto wenye umri chini ya miaka 12 kushuka chini watalipa sh. 18,500.

Treni hiyo inatarajiwa kuanza safari zake Julai mwaka huu kama ilivyotangazwa. Hivi karibuni Rais Samia alitoa alionekana kukerwa na treni hiyo kuchelewa kuanza safari na alitoa maelekezo ifikapo Julai iwe imeanza kazi.

Nauli hizo zimepitshwa na Bodi ya Wakurugenzi ya Latra kwa kuzingatia umbali kwa kilomita.

“Nauli hizi ni baada ya kufanyia kazi maombi yaliyoletwa na Shirika la Reli Tanzania (TRC) na wadau wengine,” ilieleza taarifa hiyo.

Taarifa hiyo imeeleza masharti mengine ya kuzingatia kabla ya kuanza kutumika kwa nauli hizo ni mtoa huduma (TRC) kuwa na leseni ya usafirishaji.

“Kuwa na ithibati ya usalama wa miundombinu ya reli na mabehewa, kutumia mfumo wa utoaji wa tiketi za kielekroniki, kuunganisha mfumo wa tiketi za kieletroniki na mifumo ya LATRA,” ilisema

“Nauli itakayolipwa na mtu mzima na mtoto mwenye umri zaidi ya miaka 12 ni sh 9.51 kwa kilomita, na mtoto kuanzia kuanzia miaka 4 hadi 12 atalipia sh. 34.76 kwa kilomita.