Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
UCHAGUZI wa kumtafuta Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kanda ya Nyasa umeacha mtikisiko mkubwa ndani ya chama hicho kiasi cha viongozi wa chama hicho kutumiana meseji zenye maneno makali kupitia kundi lao la WhatssAp.
Kinyang’anyiro hicho kilikuwa baina ya aliyekuwa Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (Sugu) ambaye alimbwaga Mchungaji Peter Msigwa, aliyekuwa akitetea kiti hicho kwa kura 54 kwa 52.
Kabla ya uchaguzi huo Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, alitoa kauli iliyozusha mshangao kwamba kwenye uchaguzi huo zimemwagwa fedha nyingi wakati wao hata wanapotafuta fedha kwa ajili ya kukodi vyombo vya matangaza hawazipati.
Kwenye michango yao kupitia kundi lao la WhatssAp, viongozi hao wa chama hicho wanatuma jumbe za kumwandama Mchungaji Msigwa, huku wengine wakitaka aondolewe.
“Mchungaji Msigwa hatakiwi kuwa kwenye kundi hili kuanzia sasa,” alisema mmmoja wa wachangiaji kwenye kundi hilo. Aidha, Mchgungaji Msigwa amekuwa akitakiwa aweke hadharani juu ya mambo kadhaa ikiwemo ukaribu wake na mfanyabiashara mmoja.
Aidha, wachangiaji wengine wamekuwa wakitumia maneno makali dhidi ya Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe
Mtikisiko ndani ya chama hicho ulishika kasi baada ya Mchungaji Msigwa kutangaza kukata rufaa katika chama hicho, akidai ushindi alioupata Sugu haukuwa halali.
Hata hivyo, wakati Msigwa akisema hayo, Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itifaki, Uenezi na Mambo ya Nje wa CHADEMA, John Mrema alisema kama kweli Msigwa amekata rufaa na kufuata mfumo unaotakiwa, rufaa yake itasikilizwa na kutolewa uamuzi, kwa sababu CHADEMA ni chama kinachoheshimu demokrasia.
“Bahati mbaya kama mtu amekata rufaa halafu anaanza kuzungumza mambo ya rufaa kabla haijafika alikokata rufaa ni bahati mbaya, lakini kwa hatua ya sasa kama amekata tusubiri uamuzi wa rufaa yake kwa mujibu wa taratibu,” alinukuliwa akisema Mrema.
Akizungumza Juni 3, 2024 kwenye mkutano na waandishi wa habari alioufanyia nyumbani kwake Iringa Mjini, Mchungaji Msigwa alidai kuwa mifumo ya chama imetumika kumhujumu ili asishinde, kitendo ambacho alidai kitaifanya CHADEMA kukosa uhalali wa kuikosoa CCM.
Alidai kulikuwa na mbinu chafu dhidi yake. “Nimekata rufaa kwa chama changu kuwa makatibu watatu wa mabaraza walizuiwa kupiga kura, ukiangalia kura zangu zilizoongezeka na kufikia sita, lakini wajumbe watatu walizuiwa.
“Rufaa yangu imefafanua mambo mengi sana yaliyokiukwa katika uchaguzi hata kufutwa kwa uchaguzi wa Njombe, ulikuwa mkakati wa kunihujumu ili nisishinde, lakini nimegundua sikuwa nashindana na mpinzani wangu peke yake, bali alikuwa ana nguvu nyingine nyuma yake,” alidai Mchungaji Msigwa.
Alisema alijipanga ipasavyo ikiwamo kufanya kampeni za wazi za ushindani na hoja, akizifanya kwa uaminifu mkubwa pasipo uoga ndio maana aliasisi mdahalo baina yake na Sugu.
“Mimi uchaguzi sikushindwa na siwezi kushindwa,” amesisitiza Msigwa. Sugu alipoulizwa kuhusu mpango huo, alijibu.
“Sijamsikia ingawa najua alikuwa na mkutano na waandishi wa habari, lakini niseme siwezi kuzungumzia suala hilo kwa sasa, nina kazi nyingi.”
Mchungaji Msigwa alimtuhumu pia msimamizi msaidizi wa uchaguzi huo, John Mrema kuwa alikuwa anamfanyia kampeni Sugu kinyume cha utaratibu.
Amedai Mrema alikuwa akiwaambia wajumbe kuwa ametumwa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe anataka Sugu awe mwenyekiti wa Nyasa.
“Mwanzo niliandika mmoja wa wasimamizi wa uchaguzi (John Mrema), angeondoka ili kupisha mchakato huo. “Kama CHADEMA) tunalalamikia Serikali ya CCM kwamba wasimamizi wa uchaguzi hawatendi haki, basi tulitakiwa tuwe mfano wa kuigwa, lakini katika chaguzi zetu haki haitendeki.
“Kama mimi mjumbe wa kamati kuu natoa malalamiko haya halafu hayasikilizwi ndani ya CHADEMA, nani atasikiliza ndani ya nchi yetu,”alisema. Msigwa amedai kuna watu walianza kuleta vurugu mbele ya msimamizi wa uchaguzi huo, Benson Kigaila (naibu katibu mkuu-bara), lakini hakuna hatua zilizochukuliwa na kiongozi huyo.
Kufuatia mtikisiko unaokikumba chama hicho, hivi karibuni Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimemkaribisha ndani ya chama hicho, Mchungaji Msigwa.
Kauli hiyo ilitolewa katika mkutano wa hadhara na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla. Mkutano huo ulikuwa ni wa Katibu Mkuu wa CCM, Dkt. Emmanuel Nchimbi, ambapo ulifanyika Arusha Mjini.
Makalla alisema amemwona Mchungaji Msigwa akilalamika kutokutendewa haki kwenye uchaguzi wa Kanda ya Nyasa uliofanyika Mei 29, 2024.
“Pole sana Mchungaji Msigwa, njoo Chama cha Mapinduzi kuna demokrasia tele, kuna uwazi, hicho chama hakikufai tena,” alisema Makalla.
More Stories
Kawaida apiga kura Kata ya Ipagala
Rais Samia amlilia Dkt. Ndugulile
Makada wa CHADEMA,mbaroni kwa tuhuma za kukimbia na karatasi za kura