October 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Nchimbi awataka wananchi kuwakataa viongozi wanaochochea mauaji

Na Agnes Alcardo,TimesmajiraOnline,Moshi

KATIBU Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, amewaomba watanzania kuwakataa Viongozi wa Vyama vya Siasa wanatumia majukwaa ya mikutano ya kisiasa kuchochea ugomvi, chuki na mauaji.

Akizungumza na wananchi wa Himo katika Wilaya ya Moshi Vijijini katika Mkoa wa Kilimanjaro Juni 6, 2024 kwenye siku ya pili ya ziara yake ya siku tatu Mkoani humo.

Dkt. Nchimbi amesema, viongozi wa namna hiyo hawafai katika kuliongoza Taifa, kwani wana lengo la kuligawa Taifa ikiwa pamoja na kutengeneza mazingira ya kuchochea uvunjifu wa amani.

Amesema, yupo kiongozi mmoja wa dini aliyealikwa kwenye mkutano wa kisiasa jana Juni 5, 2024 amesikika kwenye mkutano huo akihamasisha wananchi kuanza kuandaa visu, mapanga na majembe katika uchaguzi ujao na kusema kuwa, matumizi yake hayatakuwa yale yaliyozoeleka.

“Jana nilikuwa nasoma habari katika mitandao ya kijamii, nilikuwa naifuatilia mambo yanayoendelea katika mikutano ya Vyama vya Siasa, kuna kiongozi mmoja wa dini alipewa mualiko kwenye huo mkutano, nimemsikia nadhani na nyie mtakuwa mmesikia, amewaomba wananchi waanze kuandaa visu, mapanga na majembe kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao na amesema matumizi yake hayatakuwa yale mliyoyazoea.

Amesema, watu wa aina hiyo wasiyo litakia amani Taifa si wakufumbiwa mambo na kudai kuwa, watu wanaotamani nchi kumwaga damu huanza uchochozi kidogo kidogo kutengeneza mazingira ya watu kuuwana huku wakiona ni jambo la kawaida huku akiwaomba Tanzania kupitia wananchi wa Vunjo kupuuzia kauli hizo za kichochozi na kutowaunga mkono viongozi wa namna hiyo.

Aidha Dkt. Nchimbi amesema, watanzania hawapendi masuala ya kuuwana ni wapendwa amani na kusema kuwa zaidi ya miaka 20 tangu kuingia katika mfumo wa vyama vingi, Vyama vya Upinzani bado vimeonekana kutokukuwa kisiasa na kutojua  kuwa kiongozi ni pamoja na kujali maisha ya watu”

“Nimemsikiliza mtu anawaandaa watu kukaa na visu, mapanga na majembe alafu naona meza kuu wanampigia na makofi nikasema alaa kumbe hii ndiyo sera ya chama chao kuona watu wanamwaga damu, niwaombe ndugu zangu, watu wa namna hiyo siyo wa kuwafumbia macho wazomeeni kwani hawajui kwamba kuwa kiongozi ni pamoja na kujali maisha ya watu”, amesema Dktm Nchimbi.

Amesema, kuwa kiongozi ni kuwaongoza watu katika upendo na kuwaondoa katika matatizo, huku akisema kuwa endapo Kuna kiongozi wa CCM ataonekana kuchochea watu kuandaa mauaji atafukuzwa kazi siku hiyo hiyo.

“Watu hawajui tu kwamba kuwa kiongozi ni kuwaongoza watu katika upendo na kuwaondoa katika matatizo mimi naomba niwaambieni tu kuwa, endapo siku akaonekana kiongozi wa CCM na anachochea watu kuandaa mauaji kwakweli tunamfukuza kazi siku hiyo hiyo,”amesema Dkt. Nchimbi.

Aidha amesema kuwa, anatarajia kuona Vyama vya Siasa vinaweka utaratibu wa kupandisha jukwaani viongozi wenye akili timamu na si kupandisha viongozi wasiyo na sifa.

Sambamba na hayo, Dkt. Nchimbi, ameagiza, Askari wa Wanyamapori kutotumia nguvu kubwa katika shughuli zao za kikazi kwa wananchi na badala yake watumie ubinadamu.

Kauli hiyo, imekuja kufuatia taarifa iliyotolewa na Mbunge wa Himo, Dkt. Charles Kimei, ikidai kuuwawa kwa kijana mmoja aliyepigwa risasi na Askari wa Wanyamapori huku kijana huyo akidaiwa kuwa alikuwa raia mwema.

Ziara ya Katibu Mkuu, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, leo anamalizia katika Mkoa wa Moshi ikiwa ni siku ya tatu, akiwa ameambatana na Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, CPA Amos Makalla na Katibu wa NEC, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa (SUKI), Rabia Hamid Abdallah.