November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Samia asisitiza ajenda ya Nishati safi akiwa Korea

Na Mwandishi Wetu, Korea

RAIS Samia Suluhu Hassan, amemtaka Rais wa Jamhuri ya Korea, Yoon Suk Yeol, kuungana na mataifa ya Afrika katika ajenda ya ya nishati safi ya kupikia.

Rais Samia ametoa kauli hiyo jana  jijini Seoul, Korea Kusini wakati wa mkutano kati ya Korea na wakuu wa nchi za kiafrika unaolenga kuimarisha ushirikiano baina ya mataifa hayo katika biashara na uwekezaji.

Rais Samia Suluhu Hassan amesisitiza umuhimu wa ushirikiano na uwekezaji kwenye ajenda ya nishati safi ya kupikia huku akimtaka Rais wa Jamhuri ya Korea, Yoon Suk Yeol kuungana na mataifa ya Afrika katika ajenda hiyo.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Rais Samia amesema Tanzania inaukaribisha uamuzi wa Korea katika ushirikiano wa maendeleo hasa kwenye eneo la teknolojia na matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Ameongeza kwamba Tanzania inafanya kazi na kampuni za Korea katika uchimbaji wa madini ya kinywe, hata hivyo amekaribisha ushirikiano zaidi wa kampuni za nchi hiyo katika utafiti, uchimbaji na manufaa na madini ya kimkakati.

“Kwa kuwa mimi ni Rais mwanamke pekee katika chumba hiki, lazima nizungumzie ajenda ambayo ni muhimu kwa Afrika hasa kwa wanawake, na hii ni kuwekeza kwenye ajenda ya nishati safi ya kupikia,” amesema Rais Samia.

Amesema Tanzania inaunga mkono ajenda ya Afrika ya uendelevu na pia inasisitiza umuhimu wa kuwa na ushirikiano kwenye ajenda ya nishati safi ya kupikia kama mbadala wa nishati zinazotumika.

Amesema uwekezaji kwenye nishati safi ya kupikia, sio tu kutapunguza moshi na ukataji wa misitu, bali pia kutapunguza magonjwa katika mfumo wa upumuaji na kuwawezesha wanawake.

“Kuwekeza katika ajenda ya nishati safi ya kupikia Afrika, pia kunatoa fursa za kiuchumi katika kufikia suluhu ya nishati safi katika bara hili,” amesema Rais Samia

Rais Samia amesisitiza kuhusu uwekezaji kwenye ajenda hiyo ambayo amekuwa akiipigia chapuo huku akimwomba Rais wa Korea, Yeol kuungana naye kwenye ajenda hiyo muhimu kwa bara la Afrika.

“Mimi na (Akinwumi) Adesina, Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), tunafanya kazi ya kutafuta fedha kwa ajili ya ajenda hii na katika hili, tunakuomba Rais wa Jamhuri ya Korea kuungana nasi katika hili,” alisema Rais Samia.

Akifungua mkutano huo, Rais Yeol wa Korea alisema nchi yake inakusudia kuongeza uwekezaji pamoja na biashara na mataifa ya Afrika.

Amesema katika utekelezaji wa mipango yake, Korea Kusini itaingia makubaliano ya ushirikiano wa kibiashara na mataifa ya Afrika.

Ameahidi kuunga mkono mpango wa kukuza biashara baina ya mataifa hayo, kupitia Mkataba wa Eneo Huru la Biashara na kuanza ushirikiano katika sekta ya madini.

“Korea Kusini itakuza zaidi uhusiano wake na mataifa ya Afrika katika kuimarisha mifumo ya kidigitali pamoja na kushirikiana katika masuala mtambuka yanayoikumba dunia kwa sasa,” amesema Rais Yeol.

Mkutano huo wa wakuu wa nchi na Serikali umehudhuriwa na marais wa Afrika miongoni mwao akiwemo William Ruto (Kenya), Nana Akufo-Addo (Ghana), Filipe Nyusi (Msumbiji), Emmerson Mnangagwa (Zimbabwe), Paul Kagame (Rwanda) na Mokgweetsi Masisi (Botswana).  

Wengine ni Mohamed Ould Ghazouani (Mauritania), Isaias Afwerki (Eritrea), Azali Assoumani (Comoro), Alassane Ouattara (Ivory Coast), Teodoro Obiang Nguema Mbasogo (Equitorial Guinea), Joseph Boakai (Liberia) na Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed.