Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) ipo katika hatua za mwishoni za kupokea maoni ya Kanuni za Rufaa za Ununuzi wa Umma za Mwaka 2024 ili kuiwezesha Sheria ya Ununuzi Umma ya Mwaka 2023 kutekelezeka kwa ufanisi, ambapo pamoja na mambo mengine, Kanuni hizi zitatoa wigo mpana wa kuwasilisha malalamiko na rufaa.
Akiongea katika kikao kazi cha kupokea maoni ya wazabuni na wanasheria Jijini Dar es Salaam, Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Boniphace Luhende amewataka wazabuni kutoa maoni chanya ambayo yataiwezesha PPAA kupata Kanuni za Rufaa za Ununuzi wa Umma za Mwaka 2024 zinazoendana na wakati na zitakazoiwezesha Serikali kupata thamani halisi ya fedha katika sekta ya ununuzi wa Umma.
“Kwa kuwa sheria mpya ya ununuzi wa umma ya Mwaka 2023, imeelekeza shughuli zote za ununuzi wa Umma kufanyika Kieletroniki kupitia mfumo wa NeST, na kwa kuwa moduli mpya ya kupokea na kushughulikia malalamiko au rufaa zitokanazo na michakato ya Ununuzi wa Umma imekamilika, wazabuni mjitahidi kutoa maoni yatakayowasaidia kuepukana na malamiko au rufaa zisizo na ulazima kwani kufanya hivyo kutaokoa muda na kusaidia Serikali kupata thamani halisi ya fedha,” amesema Dkt. Luhende.
Pamoja na mambo mengine, Dkt. Luhende aameongeza kuwa Sheria mpya ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2023 imeboresha masuala mbalimbali ikiwepo kupunguzwa kwa muda wa kushughulikia malalamiko na rufaa zinazotokana na michakato ya Ununuzi wa Umma.
“Muda wa siku saba za kazi kwa ajili ya kusubiri malalamiko ya wazabuni kabla ya kutoa tuzo umepunguzwa na kuwa siku tano za kazi…..………sambamba na hilo muda wa PPAA kushughulikia malalamiko au rufaa umepunguzwa kutoka siku arobaini na tano hadi siku arobaini,” ameongeza Dkt. Luhende.
Kwa upande wake, Kamishina wa Sera ya Ununuzi wa Umma, Wizara ya Fedha, Dkt. Frederick Mwakibinga amesema mabadiliko ya Sheria ya Ununuzi yamekuwa yakifanyika mara kwa mara kwa lengo la kupunguza muda, kuongeza uwazi na usawa katika shughuli za ununuzi wa umma, kuongeza ushindani na kupunguza mianya ya rushwa.
“Sote tumesikia kuwa muda wa kushughulikia malalamiko na rufaa umepunguzwa na shughuli zote za ununuzi wa Umma zinafanyika kwa njia Kieletroniki na PPAA ipo katika mchakato wa kukamilisha Kanuni za Rufaa za Ununuzi wa Umma za Mwaka 2024 ambapo baada ya kukamilika zitasaidia kuboresha Sekta ya Ununuzi wa umma,” amesema Dkt. Mwakibinga.
Naye Katibu Mtendaji wa Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) Bw. James Sando amesema zoezi la kupokea maoni kuhusu kanuni za rufaa za ununuzi wa umma ni mwendelezo wa kuwashirikisha wadau wote wanaohusika na sekta ya ununuzi. “Kanuni hizi zinaandaliwa ili kuifanya sheria mpya ya Ununuzi wa Umma 2023 kutekelezwa kwa ufanisi na kuiwezesha Serikali kupata thamani ya fedha, amesema Bw. Sando
Katika kikao hicho, Wakili wa kujitegemea, Bw. James Kasusura ameipongeza PPAA kwa kazi nzuri ya kusimamia mabadiliko ya Kanuni za Rufaa za Ununuzi wa Umma ikiwa ni pamoja na muda wa kutoa maamuzi katika mashauri yanayowasilishwa katika Mamlaka hiyo.
“Tunategemea kuboresha muda, kuongeza zaidi uwazi katika tendering, na uwazi katika mfumo na watu wavione na kuvitekeleza,” alisema Bw. Kasusura
Mwaka 2004, Serikali iliifuta Sheria ya Ununuzi wa Umma Na. 3 ya Mwaka 2001 kutokana na upungufu uliokuwepo katika Sheria hiyo na kutunga Sheria Na. 21 ya mwaka 2004 ambayo ilitumika hadi mwaka 2011. Aidha, Serikali iliifuta Sheria ya Ununuzi wa Umma Na. 7 ya Mwaka 2011 na kutunga Sheria ya Ununuzi wa Umma Na.10 ya Mwaka 2023 ili kukidhi mahitaji ya sasa ambayo yalishindwa kutekelezwa na Sheria ile ya 2011.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa