November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wabunge wampongeza Rais Samia kwa kutangaza utalii nchini

Na Mwandishi Wetu, Timesmajiraonline,Dodoma

WABUNGE wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wamepongeza juhudi za Serikali za kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini kupitia filamu ya Tanznaia The Royal Tour na amaizing Tanzania iliyozinduliwa hivi karibuni Nchini China.

Wabunge hao wametoa pongezi hizo kwa nyakati tofauti janawakati wakichangia mjadala wa hotuba ya makadirio ya bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii Bungeni, jijini Dodoma jana.

Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kagera, Oliver Semuguruka, alisema juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan, Wizara ya Maliasili na Utalii na wadau wa sekta binafsi zimechangia ongezeko la watalii wa kimataifa kwa asilimia 96 kutoka watalii 922,692 mwaka 2021 hadi watalii 1,808,205 Mwaka 2023.

Aidha, amesema hata watalii wa ndani wameongezeka kwa asilimia 152 kutoka watalii 788,933 mwaka 2021 hadi kufikia watalii 1,985,707 Mwaka 2023.

Mbunge wa Viti Maalum, Mariam Kisangi, ameema kupitia filamu ya Tanzania the Royal tour idadi ya wageni wa nje wanaotembelea hifadhi zetu imekuwa kubwa na kutoa hamasa kwa watalii wa ndani kuendelea kuhamasishwa kutangaza vivutio vya nchi yao.

Ameishauri Wizara na Taasisi zake kutengeneza filamu nyingi zaidi hasa ninazolenga kuhamasisha watalii wa ndani ili idadi iendelee kuongeza kama ilivyo watalii wa nje.

Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Singida, Martha Gwau ameishauri Serikali kuendelea kuimarisha utoaji wa mafunzo ya ukarimu na utoaji huduma bora kwa wahudumu wa hoteli, viwanja vya ndege, waongoza watalii, watumishi kwenye maeneo ya hifadhi kwa kuwa ndio wanaokutana kwa mara ya kwanza na wageni wanaotembelea nchi yetu.

“Tuendelee kuimarisha huduma ili wageni wanaokuja wawe na utamaduni wa kurudi mara ya mbili, baada ya Serikali kutangaza kwa juhudi kubwa utalii wetu .

Wageni wanaokuja wanakutana na watoa huduma wa hoteli, madereva, waongoza watalii na wahudumu kwenye hifadhi zetu, lazima tusimamie mafunzo ya watumishi hawa ili wawahudumie wageni vizuri na kuwafanya warudi kila mara nchini kwetu,” amefafanua Gwau.

Gwau ameishauri Wizara na wadau wa sekta ya utalii kwa ujumla kuongeza kasi ya kutangaza vivutio vya utalii sambamba na kuona uwezekano wa kuwa na afisa dawati/mwambata wa utalii katika balozi za Tanzania katika mataifa mbalimbali.

Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Simiyu, Tunza Mijika, ameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa bajeti yenye vipaumbele vya uhifadhi wa wanyamapori, mambo kale, misistu na nyuki pamoja na kutangaza vivutio vya utalii na kusisitiza kuwa jitihada za uhifadhi wa maeneo hayo ziendelee kushirikisha wananchi katika maeneo yao.