Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online. Manyara
KATIBU Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, amewataka Viongozi wote wa Serikali kuzingatia ubinadamu wakati wa utatuzi wa migogoro na si tu kutumia sheria.
Dkt. Nchimbi ameyasema hayo leo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Stendi ya zamani ya mabasi iliyopo Wilaya ya Babati Mjini, Mkoani Manyara, wakati akisikiliza na kutatua kero za wananchi.
Amesema, Kuna maeneo mengine lazima Viongozi washiriki kusuluhisha migogoro ya wananchi ili kutoruhusu kesi kuzagaa Mahakamani, kwani wakati mwingine kusuluhisha wananchi wananchi si tu kwa ajili ya kumaliza migogoro bali pia huonesha upendo na maelewano kubaki miongoni mwa wananchi.
“Napenda kuwaomba viongozi wote wa Serikali si kila migogoro itatuliwe kisheria, wakati mwingine busara na ubinadamu vinahitajika ili kupunguza mrundikano wa kesi Mahakamani na huo ndiyo uongozi, uongozi siyo kutunisha misuli ili watu wakuone wewe nani”, amesema Nchimbi.
Aidha amewataka watumishi Serikalini wenye Mamlaka, kutumia fedha za maendeleo ya miradi zinazotolewa na Serikali kutumika ipasavyo kama ilivyo kusudiwa na si kuzihodhi na wengine kutengeneza mazingira ya rushwa ndipo wapeleke katika miradi ya maendeleo.
“Nasema wizi ni pamoja na kutotumia fedha za umma kwa kazi iliyokusudiwa, kwani hata ukiziacha benki wewe bado ni mbadhirifu, kwa hiyo nawaomba watumishi wote kila mmoja kwa nafasi yake awe na uchungu na fedha za nchi yetu, lakini pia kuwa na uchungu na Rais anayefanya kazi kubwa kuzitafuta ikiwa ni pamoja na kuzilinda ili zifike kwa wananchi”, amesema Dkt. Nchimbi.
Pia amewatoa hofu wananchi wa Babati Mjini kuwa chama kitaendelea kusimamia miradi yote ya maendeleo iliyoanzishwa na kuikamilisha kwa wakati, huku akiwataka kuendelea kuwa na Imani na CCM na kudai kuwa kazi kubwa ya CCM ni pamoja na kusimamia amani ya nchi.
Sambamba na hilo, amewakumbusha wakazi wa Babati Mjini na wananchi kwa ujumla, kuendelea kujikumbusha wajibu wa kuipenda nchi yao kwani hakuna Taifa lingine zaidi ya Tanzania ” Tuna kila wajibu wa kuendelea kuilinda, kuipigania na kuitetea nchi yetu wakati wote kwani hii nchi ndiyo tuliyoachiwa na wazazi wetu ambao ndiyo waasisi kwani wao walitukabidhi ikiwa na umoja, amani na mshikamano hivyo ni jukumu letu na sisi kuwaachia watoto wetu”, ameongeza Nchimbi.
Kwa upande wake, Katibu wa NEC, Uenezi, Itikadi na Mafunzo CCM Taifa, Amos Makalla, ametoa rai kwa wakazi wa Babati na Watanzania kwa ujumla, kuwapuuza wale wote wanaobeza maendeleo yanayofanywa na Serikali ya awamu ya sita, chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na kusema kuwa mambo mengi makubwa yaliyofanywa yanaonekana.
“Wapuuzeni wale wote wanaodai Serikali hakijafanya chochote katika kuleta maendeleo ya nchi, kwani wao hawayaoni kwa sababu wanafanya mikutano yao barabarani hivyo watayaonaje? Jamani maendeleo hayatafutwi kwa tochi”, amesema Makalla
Pia amewasisitiza wananchi hao kuendelea kuchapa kazi katika maeneo yao ili kuunga mkono jitihada za maendeleo ya nchi na kuwataka kujitokeza kwa kiasi kikubwa kujiandikisha katika daftari la mpiga kura ili kujiandaa na uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu na kukipiatia chama cha CCM ushindi.
Aidha amewahakikishia wananchi wa Manyara kuwa, kero na changamoto zote walizotoa, Serikali na Chama vimezibeba na zitafanyia kazi.
Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, amehitimisha leo ziara yake ya siku mbili mkoani Manyara ikiwa ni jumla ya mikoa miwili aliyotembelea kati ya mikoa mitano ya ziara yake, ambapo kesho anatarajia kuendelea na ziara hiyo katika Mkoa wa Arusha.
Mbali na Mikoa ya Manyara na Singida pia atatembelea Mkoa wa Kilimanjaro na kuhitimisha Mkoani Tanga, ambapo lengo la ziara hiyo ikiwa ni kukagua uhai wa chama na utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi 2020/2025.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi