November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt. Mpango ataka NEMC iongezewe nguvu

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

MAKAMU wa Rais, Dk.Philip Mpango amezindua chapisho la utafiti wa hali ya mazingira ya Pwani na Bahari Tanzania Bara huku akiagiza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuangalia mapungufu ya kisheria yanayosababisha kukosa nguvu katika usimamizi wa usafi wa mazingira ili kufanyiwa marekebisho.

Akizungumza leo kwenye Kongamano la wadau wa mazingira lililoandaliwa na NEMC, Dk.Mpango alisema miji mingi taka zimejaa kila kona na NEMC hawana meno kisheria.

“Tumepiga kelele za kutosha kuhusu usimamizi, utunzaji na usafi wa mazingira na Sheria ni kikwazo basi zitazamwe taratibu zipo, NEMC nendeni mkaangalie Sheria zenu na Taasisi zingine, mnipe mrejesho nijue tatizo ni nini,”amesema.

Amesema kwasasa athari za mabadiliko ya tabianchi zinachangia upotevu wa asilimia moja ya pato la Taifa na inakadiriwa ifikapo Mwaka 2030 kuna uwezekano wa kupoteza asilimia Tatu ya pato la Taifa kama hatua madhubuti hazitachukuliwa.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk. Immaculate Sware Semesi,
amesema kongamano hilo limewakutanisha wadau mbalimbali wa mazingira kwa lengo la kujadiliana namna Bora ya Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira ili kutoka na mikakati ya pamoja ya kuzitambua na kushughulikia kwa maendeleo endelevu ya Taifa.

“Nchi yetu na Dunia kwa ujumla inakabiliwa na changamoto za kimazingira, mfano mabadiliko ya hali ya hewa, tabianchi, upotevu wa bioanuai, uchafuzi na uharibifu wa mazingira, upungufu wa maliasili, ni ukweli unaoathiri maisha yetu ya kila siku Afya, makuzi, mahusiano, uchumi na madhara haya yatakwenda hadi vizazi vijavyo tusiposhughulikia sasa.”

“Makubaliano ya kisayansi yapo wazi kwamba hatua za haraka na madhubuti zinahitajika ili kulinda mazingira yetu,”amesema

Ameeleza kuwa mazingira ni sekta mtambuka inayohitaji nguvu ya pamoja katika usimamizi wake.

“Baraza lina jukumu la kulinda na kuhifadhi mazingira kwa mujibu wa Sheria ya mazingira namba 20 ya mwaka 2004 na limepewa jukumu la kusimamia athari za mazingira nchini zinazotokana na shughuli za kibinadamu nchini,”amesema.

Amesema usimamizi wa mazingira umeendelea kuhitaji mbinu mpya na za kimkakati kutokana na mabadiliko yanayoendelea kuwepo katika mifumo ya ikolojia na mbinu na teknolojia za uvunaji na uzalishaji.

Amefafanua kuwa katika kuelekea siku ya mazingira duniani Baraza hilo limeona ni muhimu wadau kupata elimu ya mazingira.

“Tunategemea kongamano hili litakuja na njia ya kupunguza changamoto ya mabadiliko ya tabianchi, uharibifu wa mazingira na upotevu wa bioanuai,”amesema.

Kadhalika, amesema katika kongamano hilo wadau watajadili matumizi ya nishati safi kwa Maendeleo ya nchi na jamii.

“Pia tutajadili uthibiti wa taka ngumu, plastiki na ushiriki wa sekta binafsi katika kuhifadhi mazingira, jambo jingine kupitia kongamano hili ni kuwa na jukwaa mahsusi la wadau wa mazingira nchini ili kukutana kila mwaka kuwa na mikakati yenye tija katika usimamizi wa mazingira nchini,”amesema

Amesema jukumu la ulinzi wa mazingira si ya Taasisi moja bali ushirikiano wa kila sekta.

“NEMC inathibitisha katika kujitathmini, kujiboresha na kujiimarisha katika kushauri serikali kwenye usimamizi wa mazingira nchini. Leo kutazinduliwa chapisho la hali ya mazingira ya Pwani na Bahari Tanzania Bara ambapo kazi hiyo ilifanyika NEMC kwa kushirikiana na Taasisi zingine,”amesema.

Akiwasilisha maelezo kuhusu chapisho hilo, Dk. Julius Francis kutoka Chuo Kikuu Cha Dar es salaam (UDSM amesema ni chapisho la pili kuzinduliwa katika kipindi cha mwezi mmoja na kwamba chapisho la kwanza lilihusu upande wa Zanzibar.

“Chapisho hili limeandaliwa kwa kufuata matakwa ya mkakati wa Taifa wa usimamizi wa rasilimali za Pwani na Bahari, unatoa mchango katika uandaaji wa taarifa ya mazingira na kutimiza matakwa ya mkataba wa kimataifa wa Nairobi katika usimamizi na uendelezaji wa mazingira Bahari na ukanda wa Pwani katika eneo la Bahari ya Hindi kama inavyotakiwa vyombo vingine vya kimataifa kuandaliwa taarifa kila baada ya miaka mitano au 10,”amesema.

Amesema chapisho hilo limeandaliwa na wataalamu 18 kutoka Taasisi za Serikali na limegawanyika katika sehemu kuu sita na mandhari yake ni kuelekea uchumi wa Buluu na mchango wa rasilimali za Pwani na Bahari.

“Chapisho limebeba ujumbe mahsusi katika maeneo manne kuna viashiria vinaonesha baadhi ya makazi ya viumbe yameathirika na yapo hatarini kutoweka iwapo hatua madhubuti hazitachukuliwa ili kurejeshwa katika mazingira ya awali,”amesema

Mtaalamu huyo amesema Tanzania imebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi maeneo ya Pwani na Bahari zinazotoa fursa ya kujenga uchumi wa Buluu mkubwa na endelevu kw kuunganisha mikakati ya sekta mbalimbali.

“Chapisho hili limekuja wakati muafaka ambapo nchi yetu ipo kwenye uandaaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na utekelezaji wa sera na mkakati wa uchumi wa Buluu hivyo chapisho hili ni chanzo kizuri cha taarifa za hali ya mazingira na rasilimali za Pwani na Bahari,”amesema

Amesema katika kujenga uchumi wa Buluu kunahitaji mageuzi ya kimkakati katika kusimamia rasilimali za Pwani na Bahari kwa Kila sekta na mageuzi yanahitaji kufanyika na yatachukua muda matokeo kuonekana.