November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

ATE yazindua Tuzo ya Mwajiri Bora wa mwaka 2024

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

CHAMA cha Waajiri Tanzania (ATE) kimezindua Tuzo ya Mwajiri Bora wa Mwaka 2024 yenye lengo la kutambua na kutoa tuzo kwa waajiri wenye misingi bora ya usimamizi wa rasilimali watu na biashara.

Katika Tuzo hizo, ATE imeingia Mkataba na Kampuni ya AUDITAX International, ambapo Kampuni hiyo itaratibu mchakato wa Kumtafuta mwajiri bora wa mwaka tajwa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa ATE, Suzanne Ndomba, amesema tuzo hiyo inatokana na tafiti ambazo zinamuongoza Mshauri Mwelekezi kufuatila kwa umakini mazingira ya mwajiri kama yana vigezo ambavyo vinajazwa katika dodoso.

“Tangu kuanzishwa kwake, Tuzo ya Mwajiri Bora wa Mwaka imeendelea kuwa tukio muhimu katika kalenda za waajiri nchini ambapo kwa miaka kadhaa sasa tuzo hizi zimeendelea kuhamasisha waajiri kuweka juhudi katika usimamizi wa rasilimali watu kwa kuweka misingi, kanuni na mikakati yenye mahusiano bora mahala pa kazi na kuwezesha kufanya biashara na kuleta tija na faida.”

Ndomba amesema mwaka huu kutakuwa na Tuzo ya Mshindi wa Jumla (Overall), Tuzo zinazotolewa kulingana na ukubwa kwa Kampuni, Tuzo ya waajiri bora katika Sekta binafsi Tuzo ya Waajiri katika Sekta ya Umma Tuzo za mashirika yasiyo ya kiserikali, Tuzo ya Mwajiri Bora Mzawa.

Amesema vigezo vitatu vimeongezwa kwenye orodha ya Tuzo zitakazoshindaniwa, ambavyo ni Afya na Usalama Mahala pa kazi, Mwitikio Dhidi ya VVU na UKIMWI, utengenezaji wa Ajira lakini pia Most Improved Employer, and Club of Best Performers.

Kuhusu vipengele vya utoaji wa Tuzo, kwa Mwaka 2024 Ndomba amesema vitakuwa 17 ambavyo ni pamoja na ubora katika usimamizi wa Rasilimali Watu, Tuzo ya Utofautishwaji na Ushirikishwaji, Masuala ya Utawala na Uongozi, Ukuzaji wa Vipaji, Wajibu wa Taasisi kwa jamii, Ushirikishwaji wa Mwajiriwa Usimaizi wa Utendaji, Mafunzo ya Ujuzi wa kazi na Uanagenzi, Maudhui ya Ndani, Ubora, Uzalishaji na Ubunifu, Mabadiliko ya Tabia Nchi, namna ambavyo makampuni yanakabiliana na Majanga na kuathiri ajira na kazi

Ndomba amewataka waajiri kujitokeza kwa wingi kushiriki katika mchakato huo muhimu wa kumtafuta Mwajiri Bora wa Mwaka ambaye atatangazwa rasmi katika tukio kubwa la utoaji wa Tuzo hizo ambalo litafanyika wiki ya kwanza ya Desemba mwaka huu.

Pia ameyasihi makampuni shiriki kuwasilisha madodoso mawili yaliyojazwa, moja likiwa limejazwa na Uongozi au Mkurugenzi Mkuu au Mkuu wa kitengo cha usimamizi wa Rasilimali Watu na dodoso jingine lililojazwa na mwajiriwa wa kawaida au mwakilishi wa Chama cha Wafanyakazi