November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kigoma wampongeza Samia kuwapelekea miradi wezeshi

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Kigoma

WAKAZI wa Kijiji cha Songambele katika Kata ya Mnyegera, tarafa ya Muyama Wilayani Buhigwe Mkoani Kigoma wamepongeza  Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwaletea miradi wezeshi ambayo imeleta neema kubwa miongoni mwa jamii.

Wakizungumza na waandishi wa habari waliofika kijijini hapo jana kujionea manufaa waliyopata walengwa wa TASAF katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia, wameeleza kufurahishwa na uamuzi huo, kwani umewainua kiuchumi.

Mariam Sogoti (50) mkulima mkazi wa Kijiji hicho ambaye ni mnufaika wa mpango huo ameeleza kuwa walibuni kujenga daraja la mbao linalounganisha vitongoji vya Kumsenga na Bulambila na Serikali ikawaletea zaidi ya sh mil 10.

‘Huu mradi umetusaidia sana, kwanza tumepata kipato, pili wakati wa mvua tulikuwa tunashindwa kupita kwa sababu mto ulikuwa unajaa sana maji hivyo kukwamisha shughuli zetu za kilimo lakini sasa tunapita wakati wote,” alisema.

Mzee Lulamye Midaho (80) mkulima, mkazi wa Kitongoji cha Kumsenga ameishukuru Serikali ya awamu ya 6 kwa kuendeleza mradi wa TASAF na kuwaletea miradi wezeshi inayobuniwa na wananchi wenyewe .

Alibainisha kuwa miradi hiyo imeleta neema kubwa kwa wananchi kwani imesaidia kutatua kero zao hususani za miundombinu ya barabara akitolea mfano wa daraja lao la mbao lililojengwa na walengwa wa mradi huo katika kijiji hicho.

Zwili Magendo (52) mkazi wa Kitongoji cha Bulambila amedokeza kuwa mradi wa TASAF una manufaa makubwa sana kwa wananchi, kaya nyingi hususani za vijijini zina maisha magumu sana lakini tangu kuanzishwa mradi huu wana uhakika wa kula milo 3 kwa siku.

Aliongeza kuwa miradi wezeshi iliyoanzishwa na serikali kupitia mpango huo ni mkombozi kwa wakulima kwa kuwa imewasaidia kujenga barabara na madaraja katika maeneo ambayo yalikuwa hayapitiki hivyo kupunguza kero zilizokuwepo.  

Mratibu wa TASAF wilayani Buhigwe Rojadeta Mwanri ameeleza kuwa wilaya hiyo ina jumla ya walengwa 8181 wanaonufaika na kubainisha kuwa katika kipindi cha miaka 3 ya utawala wa Rais Dkt Samia wamewezeshwa jumla ya sh bil 4.6.

Alibainisha kuwa hadi sasa jumla ya miradi wezeshi 48 imeibuliwa na wakazi wa wilaya hiyo na kutekelezwa katika vijiji vyote 44, miradi hiyo ipo katika sekta za barabara, maji, maliasili na uhifadhi wa mazingira.