November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Makamishna waliopandishwa vyeo na Rais Dkt.Samia wakumbushwa cheo ni kuongezewa majukumu

Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

KAMISHNA Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na uokoaji nchini,John Masunga(CGF) amewavisha vyeo Makamishna na Manaibu Kamishna wa jeshi la zimamoto na uokoaji waliopandishwa vyeo na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan huku akiwakumbusha kwamba kupanda cheo ni kuongezewa majukumu ya kazi hivyo wawe tayari kuzitumikia nafasi hizo.

CGF Masunga amewavisha Makamishna na Manaibu Kamishna hao vyeo hivyo jijini hapa leo Mei 30,2024 huku akiwataka Maafisa hao kuzingatia viapo vyao kutokana na majukumu waliyopewa katika kuitumikia nchi.

Amesema Makamishna hao wamepewa dhamana kubwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kutokana na kuwaami hivyo wakawe wabunifu na kuongeza Kasi ya utendaji kazi ili jeshi hilo liendelee kuwa imara katika utoani huduma.

“Kupandishwa cheo ni kuongezewa majukumu na tunapotoka hapa tufahamu kwamba tunaenda kuwatumikia wananchi Kwa kuzingatia viapo vyetu na hiyo ndiyo Dira ya jeshi la zimamoto na uokoaji,”amesema CGF Masunga.

Kwa upande wake Kamishina Utawala na Fedha wa Jeshi hilo,Mbaraka Semwanza amemshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa nishani za Vyeo hivyo huku akiahidi kufanya kazi kwa uadilifu.

Akizungumza kwa niaba ya Makamishna hao ambao wamevishwa vyeo na kula kiapo Kamishna wa Usalama kwa Umma Athumani Rwahila amesema kuwa wapo tayari kuendelea kufanya kazi usiku na mchana bila kuchoka ili kulinda uaminifu na imani waliopewa ya kuwatumikia wananchi.

“Vyeo hivi ni deni kwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan na Taifa kwa ujumla hivyo tunatakiwa kulipa deni hilo kwa kuchapa kazi kwa bidii,nidhamu na weledi zaidi,”amesema Rwahila.