November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RC Chacha aonya walimu wanaogomea uhamisho

Na Allan Vicent, TimesMajira Online , Tabora

MKUU wa Mkoa wa Tabora, Paul Matiko Chacha, amewaagiza walimu 2 wa shule ya Msingi Mabatini iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Tabora waliogoma kuripoti katika vituo vyao vipya vya kazi kuripoti haraka iwezekanavyo.

Ametaja walimu hao kuwa ni Juma Mahundi na Rose Mgaya ambao walipewa uhamisho Mei 6 mwaka huu na kutakiwa kuripoti katika vituo vipya vya kazi vilivyopo katika manispaa hiyo lakini wakagoma kufanya hivyo.

RC ametoa agizo hilo jana alipotembelea Shule ya Msingi Mabatini iliyopo katika manispaa hiyo ili kujionea maendeleo ya shule hiyo kitaaluma na kuzungumzia na walimu juu ya masuala mbalimbali ya maendeleo ya shule hiyo.

Amesema kuwa Mwalimu Rose Mgaya alihamishiwa katika Shule ya Msingi Farm Nyamwezi na Juma Mahundi alihamishiwa katika Shule ya Msingi ya Ndevelwa, katika halmashauri ya Manispaa hiyo lakini hawajaripoti hadi sasa.

Amebainisha kuwa walimu hao licha ya kutakiwa kuondoka katika kituo chao cha zamani waligoma na wanadaiwa kuwatishia viongozi wao akiwemo Mkuu wa Shule na Afisa Elimu na kulalamika kwamba wamewaonea.

RC Chacha amesisitiza kuwa mtumishi yeyote wa serikali anapaswa kufanyia kazi sehemu yoyote ile na sio kujipangia anakotaka yeye, na kuongeza kuwa serikali haitawafumbia macho watumishi wa namna hiyo kwani wanarudisha nyumba juhudi za serikali za kutoa elimu bora.

‘Kama Mkoa hatutamvumilia Mtumishi yeyote anayelipwa mshahara na serikali lakini anagoma kuripoti katika kituo cha kazi anachopangiwa, asiporipoti ndani ya muda anaopaswa kuripori kisheria atakuwa amejifukuza kazi’, amesema Chacha.

Katika kikao hicho RC Chacha amewapatia barua zao za uhamisho na kuwataka kuripoti mara moja katika vituo vyao ila kama Mwalimu Mkuu wa shule husika anatoa maamuzi mengine hiyo ni juu yao kwani wao ndio wazembe.