Na Agnes Alcardo, TimesMajira Online, Singida
KATIBU Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi amewataka wananchi wa Wilaya ya Manyoni Mkoani Singida, kuwakemea wanaotaka kuligawa Taifa kwa maslahi yao binafsi bila ya kujali umoja na mshikamano.
Dkt. Nchimbi ameyasema hayo leo katika Mkutano wa Hadhara uliofanyika eneo la Majengo katika Wilaya ya Manyoni mkoani Singida, akiwa katika ziara yake inayolenga kutembelea mikoa mitano, yenye lengo la kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020/2025, huku akiwasisitizia wananchi kuwa na umoja na kutokubali kugawanywa.
“Katika mambo ambayo naomba niwasihi leo ni kuhusu suala la kuwa na umoja, tusikubali leo aje mtu kutugawanya eti huyu wa bara na huyu wa Zanzibar hapana hii siyo Tanganyika Bali ni Tanzania na Tanzania nchi yenye upendo na amani na haibagui wananchi wake kwa kuangalia rangi, dini wala kabila.
Amesema, lengo la Serikali ni kuwahudumia wananchi wake na kutekeleza miradi yote ya maendeleo nchi nzima, huku akiahidi changamoto ya ukosefu wa umeme wilayani humo kufanyiwa kazi na kutatuliwa kwa kuweka kituo kidogo cha kupooza umeme (sub station) pamoja na ukamilishwaji wa miradi wa maji amba hadi sasa umebaki asilimia chache kukamilika.
” Hii ni nchi salama na yenye Rais msikivu ambaye ni Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, anafanya mengi sana na ndiyo Serikali ya awamu hii ya sita pekee iliyofanywa mambo mengi Mkoani Singida hadi leo hii imekuwa hivi na wengine nimewasikia hapa walisema Sasa hivi Singida ni Kama Ulaya”, amesema Dkt. Nchimbi.
Sambamba na hayo, pia amemtaka Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida, Martha Mlata, kutoa kipaumbele kwa walemavu pindi wanapogombea nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya chama na kusema kuwa, kufanya hivyo ni kutekeleza Ilani ya CCM.
” Ilani yetu ya chama kati ya mambo yaliyoahinishwa ni pamoja na kutoa vipaumbele kwa watu wenye ulemavu, hivyo nikuombee ndugu Mwenyekiti kutekeleza hili hata katika chaguzi mbalimbali ili watu Hawa waweze kupatiwa nafasi mbalimbali pindi wanapogembea nafasi mbalimbali za uongozi”, aliongeza Dkt. Nchimbi.
Kwa upande wake Katibu w NEC Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Taifa, Amos Makalla, amesema malengo ya ziara hizo zinazofanywa na CCM ni pamoja na kukutana na wananchi katika maeneo mbalimbali kusikiliza changamoto zao na kukagua utekelezwaji wa miradi.
” Malengo ya ziara zetu ni kuangalia uhai wa Chama chetu,, kutembelea wananchi na kusikiliza kero zao pamoja na kukagua utekelezwaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, lakini tangu tumefika hapa na kupokea taarifa kutoka Ofisi ya chama kwakweli hali ya kisiasa inaridhisha na tutashinda kwa kishindo katika chaguzi zote”, alisema Makalla.
Nae Mwenyeki wa CCM Mkoa wa Singida, Martha Mlata, amesema hali ya kisiasa Mkoani humo ipo shwari na miradi mablimbali ya maendeleo inaendelea kutekelezwa.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa