November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia kufanya ziara ya kikazi nchini Korea

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kufanya ziara ya kikazi ya siku sita, Jamhuri ya Korea, kufuatia mwaliko wa Rais wa nchi hiyo, Yoon Suk Yeol. Ziara hiyo itaanza Mei 31 hadi Juni 6, 2024.

Akiwa nchini humo, Rais Samia atafanya mazungumzo rasmi Ikulu na Rais wa Jamhuri ya Korea, kuhusu mahusiano kati ya nchi hizo mbili, sanjari na kushuhudia utiaji saini wa mikataba kadhaa. Moja wapo ya mikataba hiyo ni utakaohusu mkopo nafuu wa Dola bilioni 2.5 ili kusaidia miradi ya maendeleo kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

Mingine ni ushirikiano wa masuala ya anga, uchumi wa buluu, madini ya kimkakati, kilimo, utamaduni na sanaa.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa January Makamba, amesema Dkt Samia akiwa nchini humo, pia atatunukiwa Udaktari wa heshima kutoka Chuo Kikuu cha Anga Korea (KAU) kwa lengo la kutambua mchango wake wa kuleta mabadiliko, sera na uongozi wa kimantiki.

Dkt. Samia anaheshimika kwa maendeleo ya miundombinu ya viwanja vya ndege; uwekezaji katika kujenga uwezo wa mifumo na wafanyakazi nchini Tanzania.

Katika hatua nyingine, Dkt. Samia atahutubia mkutano kati ya Serikali ya Korea na wakuu wan chi za Afrika, utakaofanyika Juni 4 na 5 kwa lengo la kutoa maoni katika jopo la Kuimarisha Usalama wa Chakula na Madini, Diplomasia ya uchumi bila kusahau kikao chake na viongozi wa Kampuni Kuu za Korea ili kuangalia uwezekano wa kushirikiana katika nishati, miundombinu na utayarishaji wa filamu.