Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
SERIKALI ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imesema itaendelea kuweka mazingira rafiki na wezeshi ya kufanya biashara pamoja na kuweka sera na sheria zitakazo wezesha sekta za umma na binafsi kushirikiana kuleta maendeleo kwa taifa.
Akizungumza kwenye kikao cha Kamati Tendaji cha Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera and Uratibu),Dkt. Jim Yonazi alisema Serikali imejizatiti kuboresha mazingira ili kuvutia zaidi wawekezaji na wafanyabiashara katika sekta binafsi lengo likiwa kuinua uchumi na kuongeza pato la Taifa.
“Tumekuwa tukirekebisha sera za nchi, sheria za kodi na sheria za usajili wa makampuni haya yote yote yanalenga kuweka mazingira bora ya kuwekeza na kufanya biashara hapa nchini.”
Alisema Dkt. Yonazi ambaye alimwakilisha Katibu Mkuu Kiongozi na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Balozi, Dkt Moses Kusiluka.
Dkt. Yonazi alisisitiza kuwa Serikali inaendeleza juhudi zake pia za kuhakikisha inasogeza huduma muhimu na stahiki kwa wananchi ili kuhakikisha mazingira ya ufanyaji kazi yanakuwa na tija kwa jamii.
Naye Katibu Mtendaji wa TNBC, Dkt Goodwill Wanga amesema kuwa kupitia vikao na mikutano ya baraza wamefanikiwa kuona utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwa ni pamoja na Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara (MKUMBI) ukitekelezwa kwa asilimia kubwa.
“Tunaona Serikali inaendeleza juhudi na jitahida za kuhakikisha Watanzania wote wanafurahia huduma zinazotolewa na serikali ikiwa ni pamoja na kusomana kwa mifumo ili wanachi wapate huduma stahiki na kwa wakati,” alisema Dkt. Wanga.
Dkt. Wanga alisema Serikali inaendelea kufanya kazi kwa karibu na sekta binafsi ikiwa ni pamoja na kuondoa vikwazo vya kiutendaji, kutunga sheria na sera rafiki kwa wafanyabiashara pia kutafuta fursa za masoko makubwa ya kibiashara nje ya mipaka ya nchi.
Kwa upande wake Gavana wa Benki Kuu ( BoT), Emmanuel Tutuba, alisema kuwa sekta ya fedha imendelea kuimarika na kutoa mchango stahiki kwa sekta za umma na binafsi kwa kuhakikisha zinakuwa na ufanisi mkubwa na wenye tija kwa pato la Taifa.
“Tunapenda kuona wananchi wakichangamkia fursa ambazo kama Benki Kuu tunazitoa ikiwa pamoja na utoaji wa mikopo nafuu ambayo itasaidia kuleta ustahimilivu wa mitaji na miradi wanayoiendesha.”Alisema GavanaTutuba
Naye Mwenyekiti wa Kongani ya Madini kutoka sekta binafsi, Bw Simon Shayo amesema kuwa kama sekta binafsi wanajivunia kuona kuwa serikali inaweka juhudi katika kutatua hoja ambazo zinaibuliwa na wafanyabiashara lakini pia kuongezeka kwa ubia na mjadala chanya kati ya serikali na sekta binafsi.
“Wito wetu kwa Serikali ni kuwaomba waendelee kufanyia kazi changamoto na mapendekezo yote yanayotolewa na sekta binafsi na wafanyabiashara kwa ujumla kwa ujumla wake,” alisema Shayo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Chemba ya Wafanyabiashara Wenye Viwanda, Biashara na Kilimo Tanzania (TCCIA), Oscar Kisanga alisema kuwa Serikali imekuwa ikiwashirikisha kwa ukaribu sekta binafsi katika kujadili changamoto mbalimbali zinazo wakumba katika utendaji na kuwasaidia utatuzi wake.
“Tunaahidi kuendelea kutoa mchango na ushirikiano wetu wa karibu kwa serikali katika kuhakikisha juhudi zinazofanyika zinazaa matunda na kufikia hatima tunayoikusudia,alisema Bw Kisanga.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa