December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Dkt. Samia atajwa kwa mchango wake mkubwa sekta ya mifugo

Na. Stephen Noel, Kagera

Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameweka historia ya kutafsiri ndoto halisi ya wingi wa mifugo nchini katika kubadilisha mfumo wa maisha kwa watanzania kupitia sekta hiyo.

Akizungumza wakati wa hafla fupi ya kuwaonesha vijana wanaohitimu mafunzo ya unenepeshaji mifugo kupitia Programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT – LIFE), inayosimamiwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, vitalu watakavyopatiwa kwa ajili ya ufugaji katika Ranchi za Kagoma na Kitengule zinazosimamaiwa na Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO), Mkuu wa Wilaya ya Karagwe ,Julius Laizer amesema Rais ameweza kuirasimisha rasmi biashara ya mazao ya mifugo kwa kuwa Sekta ya Mifugo ni muhimu katika maisha ya binadamu.

Akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Laizer amesema ni vigumu kutenganisha biashara yoyote inayohusu chakula cha binadamu isifanikiwe, hivyo kuwataka vijana wa BBT – LIFE kusimamia vyema ndoto na maono ya Rais Samia kwa kuwa wapo sehemu sahihi katika kujifunza na kufuga mifugo kibiashara.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Daniel Mushi amesema wizara inawaangalia vijana hao kama waleta mapinduzi kwenye Sekta ya Mifugo hivyo imeamua kuwaunganisha na baadhi ya benki zilizopo nchini kupata fursa za mikopo.

Aidha, amesema Rais Samia katika diplomasia ya kiuchumi amekuwa akizunguka nchi mbalimbali kutafuta masoko ya mazao ya mifugo na uvuvi ambapo kwa sasa nchi inahitaji wawekezaji wakubwa katika sekta hizo ili kuvipatia viwanda vilivyopo nchini mifugo kwa ajili ya kuchakatwa na kuhudumia masoko ya kimataifa, ambapo pia vijana wa BBT – LIFE wanatakiwa kuwa wawekezaji wakubwa katika Sekta ya Mifugo.

Pia, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO), Bwire Mujarubi amesema kwa mujibu wa mwongozo kampuni hiyo imepewa majukumu ya kutenga vitalu kwa vijana wa BBT – LIFE, kupanga vijana hao kwenye vitalu, kuwapatia mikataba wafugaji katika ranchi za NARCO na kuwa miongoni mwa wateja wa mifugo kutoka kwa vijana wa BBT – LIFE watakaopatiwa vitalu katika ranchi hizo.

Amesema licha ya awamu ya kwanza ya BBT – LIFE kuelekea mwishoni ifikapo Tarehe 30 Mwezi Juni mwaka huu, NARCO itaendelea kuwalea vijana hao 161 ambapo kila mmoja atapatiwa ekari 10 bila kulipa gharama za upangaji katika kipindi cha miaka mitano kwenye ranchi za Kagoma hekta 311 na Kitengule hekta 2,000 zilizopo Wilaya ya Karagwe Mkoani Kagera.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Mafunzo ya Mifugo nchini (LITA) Dkt. Pius Mwambene amesema kwa kipindi cha miaka miwili ambacho vijana wa BBT – LIFE wamekuwa wakipata mafunzo katika wakala hiyo wamepata uzoefu mkubwa wa kuandaa miundombinu ya mifugo pamoja na biashara ya mifugo.

Pia, amesema lengo la programu hiyo ni kukuza ufugaji wa mifugo wenye tija kwa kuandaa vijana kuwa wawekezaji wakubwa kwenye sekta hiyo na kwamba programu hiyo kwa sasa itapelekwa kwenye ngazi za serikali za mikoa ili kuwanufaisha vijana wengi zaidi.

Mmoja wa vijana wanaonufaika na programu ya BBT – LIFE,Posper Mgalu amewaasa vijana wenzake kushirikiana ili kufikia malengo ambayo serikali imekusudia na kuwa chachu ya vijana wengine kujiunga na mafunzo kwa awamu ya pili na kufuga kibiashara kwa kuwa Sekta ya Mifugo ina soko kubwa ndani na nje ya nchi.

Wizara ya Mifugo na Uvuvi imekuwa ikiendesha mafunzo ya unenepeshaji mifugo katika vituo vya Wakala ya Mifugo nchini (LITA) na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) kupitia Programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT – LIFE) ili kufikia maono ya Rais Dkt. Samia ya kuwawezesha vijana kufanya ufugaji wenye tija katika sekta za mifugo na uvuvi.