Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Saadi Mtambule amewataka wananchi wa Wilaya ya Kinondoni hususani Kata za Kawe, Kunduchi, Wazo na Mbezi Beach kujitokeza kunufaika na fursa ya kuunganishwa bure kwenye huduma ya uondoshaji majitaka kupitia utekelezwaji wa mradi wa Usafi wa Mazingira Mbezi Beach unaosimamiwa na Mamlaka ya Majisafi na usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA)
Akizungumza wakati wa kikao cha viongozi wa Wilaya ya Kinondoni iliyohusisha kutembelea na kukagua utekelezaji wa mradi wa Usafi wa Mazingira Mbezi Beach pamoja na kuzindua kampeni ya mguu kwa mguu uunganishwaji wa huduma ya Majitaka Kaya kwa Kaya, ambapo Mhe. Mtambule amesema kuwa hakuna hata mwananchi anaepaswa kukwepa kufanyiwa maunganisho ya huduma hii kwa kuwa itasaidia kuondoa gharama na changamoto za uondoshaji wa majitaka kwa njia na hivyo kuboresha mazingira.
“Mimi niwatake kila mwananchi ambae amepitiwa na mradi huu ahakikishe anajisajili ili aweze kuunganishwa kwenye huduma hii inayolenga kupunguza uchafuzi wa Mazingira na kuboresha afya za wananchi kwa asilimia kubwa, hizi ni jitihada za Serikali inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa fedha ili wananchi waunganishwe bure kwenye huduma za majitaka,” amesema Mhe Mtambule.
Amewataka wanufaika wote wa mradi kuwa waangalifu wa miundombinu ya mradi kwa kuepuka kuharibu ili mradi ambao utadumu kwa muda mrefu ulete tija kwa wananchi na uweze kutekelezwa kwenye Kata nyingine za Wilaya ya Kinondoni.
Ametumia nafasi hiyo kuwasihi Wenyeviti wa mtaa na watendaji wote wa mtaa kutoa elimu kwa kina kwa wananchi wote ili wajue manufaa ya mradi huu na umuhimu wa kufanya maunganisho ya huduma hii.
Mwakilishi wa Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), Mkurugenzi wa Miradi Mhandisi Ramadhani Mtindasi amesema kuwa mradi huuu wa kisasa na wa kipekee Nchini na Afrika Mashariki kutokana na ubora wake wa kuondosha majitaka majumbani na kuchakata kwenye Mtambo.
Ameongeza kuwa kwa sasa mradi umefikia hatua nzuri ya kuanza kufanya maunganisho ya mifumo ya majitaka kwa wateja wapatao 11,000 wa Kata za Kawe, Kunduchi, Wazo na Mbezi Beach bure.
“Zoezi la maunganisho ya huduma hii litaanza hivi karibuni na wananchi watapewa taarifa kupitia ofisi za Serikali za mitaa, hivyo wananchi watapata utaratibu wote wa namna ya kupata huduma hii kikamilifu,” ameeleza Mhandisi Mtindasi.
Mradi wa Usafi wa Mazingira Mbezi Beach unatekelezwa na kusimamiwa na DAWASA kupitia Mkandarasi wa Kampuni ya Beijing Construction Engineering Group na Kampuni ya Metito Overseas kwa gharama ya bilioni 124, ukihusisha ujenzi wa vituo viwili vya kusukuma majitaka, ulazaji na uchimbaji wa mabomba kwa umbali wa kilomita 101, pamoja na ujenzi wa chemba 2,383 za kukusanya majitaka. Mradi unalenga kunufaisha wakazi 11,488 wa Kata ya Wazo, Mbezi Beach, Kawe na Kunduchi.
More Stories
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu