October 7, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Katibu Mkuu UWT apokelewa Dodoma,asisitiza wanawake kujitokeza kugombea

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

KATIBU Mkuu wa umoja wa wanawake Tanzania (UWT)Suzan Kunambi(MNEC)amewataka wanawake wa Chama cha Mapinduzi kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwaka 2025.

Suzan amesema hayo jijini hapa leo Mei 24,2024 wakati akizungumza baada ya kupokelewa alipowasili jijini hapa katika Makao Makuu ya umoja huo ambapo katika mapokezi hayo viongozi mbalimbali wameshiriki wakiongozwa na Mwenyekiti wa umoja huo Mary Chatanda,Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,Rosemary Senyamule pamoja na wa bunge wanawake.

Amesema kuwa licha ya kuhamasishana wanawake kwenda kupiga kura lakini wanapaswa kujitokeza kugombea pia.

Aidha amesema kuwa maono ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ni makubwa sana katika maendeleo hivyo amewataka wanawake wa UWT kuyaelezea mazuri yanayofanywa na viongozi hadi yaeleweke ili yaache alama katika jamii.

“Naomba mnipe ushirikiano ili tuweze kutekeleza majukumu yetu na tuache alama zitakazoonekana vizazi na vizazi,”amesema Suzan.

Hata hivyo amewataka UWT kuhakikisha CCM inashinda maeneo yote katika uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika mwaka huu .

“Tunaanza na Serikali za mitaa tutahakikisha maeneo yote tunashinda ni lazima tukasake kura za CCM iwe jua iwe mvua na viatu au bila viatu lazima tushinde,”amesema Suzan.

Suzan aliteuliwa Mei 9,2024 baada ya Kamati kuketi chini ya Makamu Mwenyekiti wake ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Hussein Ali Mwinyi katika kikao chake maalum kilichofanyika Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar na kufanya uteuzi kwa niaba ya Halmashauri kuu ya chama hicho.