October 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

JKT Ruvu yaunga mkono juhudi za Rais Samia za kutangaza utalii

Na Omary Mngindo, Timesmajiraonline,Ruvu

JESHI la Kujenga Taifa (JKT) Kambi ya Ruvu iliyopo Mlandizi Kibaha Vijijini Mkoa wa Pwani, imeunga mkono juhudi za Rais Dkt. Samia Saluhu Hassan, katika suala zima la kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii.

Hatua hiyo inatokana na kambi ya Ruvu kuanzisha kitalu cha kuhifadhia wanyama kwa kutenga eneo lenye ukubwa wa ekari 70, pembezoni mwa kambi. Kwenye eneo hilo wameanza kwa kuweka wanyama aina Twiga, Swala, Pundamilia na wengine wadogowadogo.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Kikosi hicho Kanali Peter Mnyani, mbele ya Mkuu wa Wilaya, Nickson John, wakati wa uzinduzi wa zuu hiyo.

“Mkuu wa Wilaya uanzishwaji wa zuu ya wanyama ni kulenga kuunga mkono juhudi za Rais Samia, ambaye amedhamiria kuifungua nchi katika sekta mbalimbali.

Pia tunakumbuka alizindua filamu ya Royal Tour iliyochangia kupatikana kwa watalii wengi,” amesema Mnyani.

Kanali Mnyani aliongeza kuwa Juni, mwaka huu wanataraji kupeleka kwenye zuu hiyo Simba, ambaye hatokuwa na madhara kwa wanamchi wataokwenda kuangalia wamyama hao.

wa upande wake DC Nickson alipongeza ubunifu huo unaolenga kuwawezesha wananchi wa Kibaha na maeneo mbalimbali kufika kujionea wanyama hao, ambao wengine huwangalia kupitia luninga.

“Uwepo wa zuu hii utasaidia wananchi wa Kibaha, lakini si wao tu ukizingatia ipo mita chache kutoka Barabara Kuu ya Dar es Salaam kuelekea mikoani, hapa abiria wanaopita eneo hili wanaweza kuja uangalia wanyama hawa,” amesema