November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wizara ya Afya yaja na vipaumbele kumi bajeti 2024/25

Na Joyce Kasiki, TimesmajiraOneline, Dodoma

WAZIRI wa Afya Ummy Mwalimu, amesema wizara hiyo imejiwekea vipaumbele 10 inavyotarajia kuvitekeleza katika mwaka wa fedha wa 2024/2025 kwa lengo la kuboresha huduma za afya nchini.

Hayo yalielezwa Bungeni Jijini Dodoma na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, alipokuwa akiwasilisha hotuba ya mapato, makadirio ya matumizi kwa mwaka wa fedha 2024/25.

Aidha, alipongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa hatua mbalimbali anazochukua kuboresha huduma za afya kwa Watanzania, ikiwemo kupungumza vifo vitokanavyo na uzazi.

Alitaja vipaumbele hivyo kuwa ni pamoja na kuimarisha huduma za kinga dhidi ya magonjwa, kuimarisha upatikanaji na ubora wa huduma za afya zinazotolewa na vituo vya kutolea huduma za afya kuanzia ngazi ya zahanati hadi Taifa, kuimarisha mifumo ya ugharamiaji wa huduma za afya nchini.

Vipaumbele vingine ni kuimarisha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto ili kupunguza vifo vya wajawazito na watoto wachanga, kuimarisha upatikanaji na uendelezaji wa wataalam katika sekta ya afya kwa fani za kati, ubingwa na ubingwa bobezi, kuimarisha huduma za matibabu ya ubingwa na ubingwa bobezi nchini,
kuendeleza na kusimamia afua za Tiba Asili na Tiba Mbadala.

“Lakini pia Kuimarisha upatikanaji wa huduma za magonjwa ya kuambukiza, magonjwa yasiyoambukiza na magonjwa ya mlipuko, kuimarisha huduma za afya ya akili, huduma za utengamao hususan kwa watoto, wazee na watu wenye ulemavu na kusimamia tafiti na matumizi ya matokeo ya tafiti mbalimbali za afya,”alisema Waziri Ummy.

Kadhalika, alisema kwa mwaka 2024/25, Wizara imekadiria kutumia kiasi cha sh. 1,311,837,466,000 kutekeleza vipaumbele hivyo kwa kutumia afua 89 katika kuimarisha huduma za kinga dhidi ya magonjwa ambapo kiasi cha sh. 117,611,588,304.00 kimetengwa zitakazotekeleza afua mbalimbali.

Alitaja afua hizo ni pamoja na kuendelea kuimarisha utekelezaji wa afua za chanjo kwa kuwafikia watoto 3,117,564 wenye umri chini ya miaka miwili, wasichana 871,429 wenye umri wa miaka tisa na wajawazito 3,298,437 (sh. 115,369,238,904.00) na kutekeleza afua za lishe ikiwa ni pamoja na kuendelea kuhimiza unyonyeshaji na ulishaji sahihi wa watoto.

Alisema afua nyingine ni elimu ya lishe kwa jamii na kuimarisha mpango wa kuongeza virutubishi kwenye vyakula, ambapo ununuzi na usimikaji wa mashine 300 za kuongeza virutubishi (Dozifiers) utafanyika (Shilingi 1,607,700,000.00) na kimarisha utekelezaji wa afua za usafi na afya mazingira katika jamii, mipakani, taasisi za umma na binafsi ikiwemo kutekeleza kampeni ya mtu ni afya awamu ya pili.

Kuhusu eneo hilo, Ummy alisema Wizara imeendelea kuimarisha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini ili kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG 2030) ya kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kufikia chini ya 70 kwa kila vizazi hai 100,000, vifo vya watoto walio chini ya miaka mitano kufikia 25 kwa kila vizazi hai 1000 na vifo vya watoto wachanga kufikia 12 kwa kila vizazi hai 1000 ifikapo mwaka 2030.

Ummy alisema katika mwaka 2023/24 Sekta ya Afya imefanya uimarishaji wa huduma mbalimbali zikiwemo huduma kabla ya ujauzito, huduma wakati wa uchungu na kujifungua, huduma baada
ya kujifungua, huduma kwa watoto, afya ya uzazi kwa vijana wa rika balehe, na huduma za masuala ya kijinsia.

Alisema uwekezaji mkubwa ambao Serikali ya Awamu ya 6 imeufanya katika eneo hili ni pamoja na utekelezaji wa afua mbalimbali vimechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kwa asilimia 80 kutoka 556 mwaka 2015/16 hadi 104 kwa kila vizazi hai 100,000, kupunguza vifo vya watoto walio chini ya miaka mitano kutoka 67 mwaka 2015 hadi 43 kwa kila vizazi hai 1000, kupunguza vifo vya watoto wachanga kutoka 25 hadi 24 kwa kila vizazi hai 1000 kwa mujibu wa utafiti wa TDHS ya mwaka 2022.

“Mwenendo huo wa kupungua kwa vifo vitokanavyo na uzazi na vile vya watoto chini ya miaka mitano inaonesha kuwa nchi yetu ipo kwenye mwelekeo mzuri katika kufikia malengo ya kidunia ifikapo 2030. Hali ya vifo vitokanavyo na uzazi kwa nchi za Afrika Mashariki na zile zinazotuzunguka ni kama ifuatavyo, Uganda 189 (UDHS 2022), Burundi 494 (UN 2023), Kenya 530.

Vingine ni kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.

Alisem Wizara imeendelea kupanua huduma za kuzuia maambukizi ya
VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kwa kujumuisha huduma za kuzuia maambukizi ya Kaswende na Virusi vya Homa ya Ini aina ‘B’ katika afua hizo.

“Lengo la kujumuisha huduma hizo pamoja ni kutumia rasilimali za kuzuia maambukizi ya VVU kutokomeza maambukizi ya Kaswende na
Virusi vya Homa ya Ini aina ‘B’ kwa watoto,”alisema

Takwimu zinaonesha kwamba, jumla ya vituo 7,830 sawa na asilimia 96 ya vituo 8,164 vinavyotoa huduma za Afya ya Uzazi na Mtoto viliweza kutoa huduma za kuzuia Maambukizi ya VVU na Kaswende kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.

Aidha alisema jumla ya wajawazito 1,453,235 sawa na asilimia 97.4 ya wajawazito 1,492,931 waliohudhuria kliniki walipimwa VVU katika kipindi cha Julai 2023 hadi Machi 2024 ikilinganishwa na Wajawazito 1,627,685 sawa na asilimia 98.9 ya wajawazito 1,645,417 waliopimwa katika kipindi kama hicho mwaka 2022/23 Wajawazito 43,323 sawa na asilimia 2.98 ya wajawazito wote walibainika kuwa na maambukizi ya VVU kwa kipindi cha Julai 2023 hadi Machi 2024 ikilinganishwa na wajawazito 47,475 sawa na asilimia 2.85 waliobainika kuwa na maambukizi ya VVU kwa kipindi kama hicho mwaka 2022/23.

Kwa mujibu wa Ummy katika kipindi cha Julai 2023 hadi Machi 2024, wajawazito 38,951 sawa na asilimia 90 ya wajawazito waliobainika kuishi na maambukizi ya VVU waliunganishwa na huduma za matibabu ya dawa za kufubaza VVU (ARVs) ikilinganishwa na wajawazito 43,208 sawa na asilimia 91 ya wajawazito 47,475 waliobainika waliunganishwa na huduma za matibabu ya VVU kwa kipindi kama hicho mwaka 2022/23.