November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RC awatahadharisha vijana wa JKT dhidi ya uhalifu

Joyce Kasiki,Timesmajira online,Kasulu

MKUU wa mkoa wa Kigoma Kamishina Jenerali Mstaafu wa Jeshi la Zimamoto Thobias Andengenye amefunga mafunzo ya vijana wa kujitolea wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) operesheni ya miaka 60 ya ya JKT katika kikosi cha Jeshi 825 Mtabila huku akiwaasa vijana hao kutokubali kulaghaiwa na kujiunga katika vikundi vya kihalifu.

Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo Mkuu huyo wa mkoa alisema kufanya hivyo itakuwa ni usaliti wa kiapo chao na Taifa ambalo limetumia gharama kubwa kuwaandaa hadi kufikia hatua ya kuhitimu mafu zo hayo.

Amesema serikali inaamini baada ya kumaliza mkataba wao JKT maisha yao yataenda kuwa mazuri kwani wamejifunza namna ya kujikwamua kiuchumi.

Amewataka kwenda kushiriki katika shughuli mbalimbali za uzalishaji mali kutokana na mambo mengi waliyojifunza katika mafunzo yao.

Naye Mkuu wa Tawi la Lojistiki na Uhansisi Jeshini Meja Jenerali Hawa Kodi ambaye alimwakilisha Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Jacob Mkunda ,amewataka vijana hao wakawe hodari wakati wote kwa kujiepusha na vitendo vitakavyowasababishia matatizo ya afya ya mwili au afya ya akili.

Naye Mwakilishi wa Mkuu wa JKT Meja Jenerali Rajab Mabele,Mkuu wa Tawi la Utawala JKT Brigedia Jenerali Hassan Mabena amewataka vijana hao kwenda kuwaelimisha wengine umuhimu wa mafunzo ya JKT na kutumia fursa hizo kuomba pindi yanapotangazwa.

Kwa upande wake Kamanda Kikosi 825 Mtabila Luteni Kanali Patrick Ndwenya amewaasa vijana hao kuwa waadilifu,uaminifu na uhodari katika kutekeleza kwa weledi majukumu watakayopewa na nchi.
Xxxx