November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwandishi wa habari mbaroni kwa kujifanya Ofisa usalama wa Taifa

Na Moses Ng’wat,Timesmajiraonline,Mbozi.

JESHI la Polisi Mkoa wa Songwe limemkamata mwanaume mmoja (jina limehifadhiwa kwa sababu maalum za kipolisi), mwenye umri wa miaka 41, Mkazi wa Magomeni Jijini Dar es salaam kwa tuhuma za kujifanya ofisa usalama wa Taifa .

Mtuhumiwa huyo ambaye ni mwandishi wa habari, inadaiwa akiwa katika mikoa mbalimbali, ukiwemo Mkoa wa Songwe alijitamnulisha kuwa ni ofisa usalama wa Taifa kutoka Ikulu ndogo Dar salaam kwa lengo la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kutoka kwa watu wanaotarajia kugombea nafasi mbalimbali kuelekea kipindi cha uchaguzi wa 2024 na 2025.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mei 5,2024,Kamanda wa polisi Mkoa wa Songwe, Augustino Senga amesema  mtuhumiwa alikamatwa Aprili 13, 2024 katika Mtaa wa Majengo mapya, Wilayani Momba.

“Mtuhumiwa huyu kabla ya kukamatwa alikuwa amepita katika mikoa mbalimbali na kujitambulisha kuwa ni ofisa usalama wa Taifa kutoka Ikulu ndogo Dar es salaam na kukutana na watu wanaotarajia kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kuelekea katika kipindi hiki cha uchaguzi ” amesema Kamanda Senga.

Kamanda Senga ameitaja mikoa ambayo mtuhumiwa huyo anadaiwa kupita na kufanya utapeli kwa watu wanaotarahia kugombea nafasi za uongozi katika chaguzi za 2024 na 2025 kabla ya kukamatwa Mkoni Songwe  kuwa ni Dodoma, Iringa, Njombe, Mbeya na Songwe.