November 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wananchi 12,000 Kilindi kupata maji ya uhakika

Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Kilindi

Mradi wa uboreshaji huduma ya maji kwenye Kata ya Bokwa, Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga, utahudumia wakazi wa vijiji vitatu vya Bokwa, Kwastemba na Kwamwande vyenye wakazi zaidi ya 12,000.

Mradi huo ni jitihada za Serikali kupitia Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Kilindi za kuhakikisha wanasogeza huduma ya maji karibu ya wananchi.

Tenki la maji la lita za ujazo 10,000 kwenye mradi wa uboreshaji maji Kata ya Bokwa

Akisoma taarifa ya mradi huo Aprili 18, 2024 kwa Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa mwaka huu Godfrey Mnzava, Meneja wa RUWASA Wilaya ya Kilindi Mhandisi Alex Odena amesema, mradi huo unatekelezwa kwa fedha za Mfuko wa Maji na kusimamiwa na RUWASA.

Huku chanzo cha maji cha mradi huo ni Mto Kwedikawa wenye uwezo wa kuzalisha maji lita 950,400 kwa siku.

“Mradi huu unatekelezwa na mkandarasi M/S Federick Construction Co. Ltd
kupitia mkataba namba AE-102/2021-2022/TAG/W/65 wenye thamani ya milioni 765.2 unaohusisha ujenzi wa miradi miwili, ambayo ni mradi wa maji Mafulila kwa gharama ya milioni 473.7 na mradi wa maji Bokwa kwa gharama ya milioni 291.4,”.

Ambapo mradi huo utahudumia wakazi wa vijiji vya Bokwa wapatao 4,404,Kwastemba 4,015 na Kwamwande 3,634 huku ujenzi wake ulianza kutekelezwa kwa mwaka wa fedha 2021/2022 Desemba 29, 2021 na unatarajiwa kukamilika Juni 30, 2024 ambao umefikia asilimia 80 ukihusisha kazi mbalimbali.

Mhandisi Odena ametaja kazi hizo kuwa ni
ujenzi wa nyumba ya mitambo (Pump house) asilimia 80, ununuzi wa bomba, uchimbaji mtaro, ulazaji na uunganishaji wa mabomba hadi kwenye tanki la maji lililopo urefu wa mita 1,176 asilimia 98.

Pia ujenzi wa tanki la kukusanyia maji (Sump well) mita za ujazo10 (lita 10,000) asilimia 80, ujenzi banio la maji (Intake) asilimia 100, ujenzi wa valvu chemba asilimia 80, ujenzi wa fensi kuzunguka nyumba ya mitambo, tanki la kukusanyia maji na chujio la maji asilimia 80 pamoja na uingizaji wa umeme wa TANESCO asilimia 30.

“Mradi huu hadi kukamilika kwake utagharimu sh. 291,459,864, ambapo mpaka sasa mkandarasi amelipwa sh 90,340,806 kwa kazi alizotekeleza na utakapokamilika utawezesha wananchi wapatao 12,052 kupata maji safi na utaongeza masaa ya kupata huduma ya maji kutoka masaa manne kwa siku hadi masaa nane kwa siku,” amesema Mhandisi Odena.

Nyumba ya mitambo (pump house) mradi wa uboreshaji maji Kata ya Bokwa

Kwa upande wake Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa mwaka huu Godfrey Mnzava amesema dhamira ya Rais Dkt. Samia ni kusogeza huduma ya maji karibu na wananchi, hivyo fedha za miradi ya maji zinazopelekwa kwa wananchi zioneshe matokeo chanya ili kutimiza adhima ya kumtua mama ndoo kichwani.

Ujenzi wa chujio mradi wa uboreshaji huduma ya maji Kata ya Bokwa
Meneja wa RUWASA Wilaya ya Kilindi Mhandisi Alex Odena (katikati) akitoa maelezo kwa Meneja wa RUWASA Mkoa wa Tanga Mhandisi Upendo Lugongo (kulia) kwenye chanzo cha maji mradi wa uboreshaji maji Kata ya Bokwa. Ni muda mfupi kabla Mwenge wa Uhuru haujafikishwa kwenye mradi huo. Wengine ni Ofisa Maendeleo ya Jamii Wizara ya Maji Sophia Swai (kushoto), Mhandisi Kitengo cha Usambazaji Maji Vijijini Wizara ya Maji Fatma Ngano (wa pili kushoto), na Mhandisi wa RUWASA Wilaya ya Kilindi Martin Malulu (wa pili kulia)
Chanzo cha maji mradi wa uboreshaji huduma ya maji Kata ya Bokwa