November 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ulega:Uzalishaji wa maziwa umeongezeka hadi lita bilioni 3.4 nchini mwaka 2022/23



Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

WIZARA ya Mifugo na Uvuvi imesema katika miaka 60 ya Muungano Uzalishaji wa maziwa umeongezeka kutoka lita 334,000 mwaka 1964 hadi lita bilioni 3.4 mwaka 2022/2023 na usindikaji wa maziwa umeongezeka kutoka wastani wa lita 41,026,000 kwa mwaka 1964 hadi wastani wa lita milioni 75.9 kwa mwaka 2023.

Hayo yameelezwa jijini hapa leo,Aprili 16,2024 na Waziri wa Wizara hiyo  Abdullah Ulega wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio yaliyopatikana katika miaka 60 ya Muungano ambapo amesema Viwanda vya kusindika maziwa pia vimeongezeka kutoka viwanda saba vya umma mwaka 1974 hadi kufikia viwanda vya sekta binafsi 105 mwaka 2023.

Aidha amesema Uzalishaji wa nyama umeongezeka kutoka tani 97,000 mwaka 1964 hadi tani 738,166 mwaka 2023.

“Hii imetokana na kuongezeka kwa viwanda vya kusindika nyama kutoka kiwanda kimoja mwaka 1964 (Tanganyika Parkers) kilichokuwa na uwezo wa kuchinja ng’ombe 800 kwa siku hadi viwanda 11 vyenye uwezo wa kusindika tani  337 kwa siku. 

“Kwa kipindi cha miaka mitatu (3) ya hivi karibuni, Mauzo ya nyama nje ya nchi yameongezeka kutoka tani 1,774 mwaka 2020/21 hadi kufikia tani 14,701 mwaka 2022/23,hivyo kufanya jumla ya tani 35,297 zenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 146.43 zilizouzwa nje ya nchi.

Amesema kuwa Katika kipindi cha mwaka 1961 – 1988 shughuli za uvuvi katika maeneo yote ya uvuvi nchini zilikuwa zikifanywa na wavuvi wadogo hivyo idadi ya wavuvi imeongezeka kutoka wavuvi 75,621 mwaka 1995 waliokuwa wanatumia vyombo vya uvuvi 22,976 hadi wavuvi 198,475 waliotumia vyombo 58,820 mwaka 2023.

Aidha, amesema kiasi cha samaki kilichozalishwa na nguvu hiyo ya uvuvi (wavuvi na vyombo)kiliongezekakutoka tani 255,900.74 za samaki zenye thamani ya TShs.  70,467,575.96 mwaka 1995 hadi tani 479,976.6 zenye thamani ya shilingi trilioni 3.4 mwaka 2023 sawa na ongezeko la asilimia 87.56. Kwa ujumla uzalishaji wa samaki umeonekana kuongezeka hali inayoashiria kuboreka kwa shughuli za uvuvi na maisha ya wavuvi wadogo nchini.

Vilevile amesema katika miaka 60 ya Muungano Serikali ya Jamhuri ya Tanzania na Serikali ya Muungano Zanzibar zilishirikiana kutokomeza ugonjwa wa Sotoka (Rinderpest), Magonjwa yaenezwayo na Kupe na Udhibiti wa Magonjwa yaenezwayo na Mbung’o.

Vilevile amesema Tanzania iliridhia kuanzisha Ukanda wa Uchumi wa Bahari (Exclusive Economic Zone-EEZ) mwaka 1989. Uvuvi wa kibiashara katika EEZ ulianza mwaka 1998 ambapo leseni zilikuwa zikitolewa upande wa Tanzania Bara na hivyo, kupelekea kuwa na hitaji la kuanzisha chombo maalum cha Muungano cha kusimamia na kuendeleza rasilimali za uvuvi zilizopo katika EEZ na Bahari Kuu ambapo Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu (DSFA) ilianzishwa rasmi mwaka 2010.

“Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu  (Deep Sea Fishing Authority-DSFA) ni Taasisi ya Muungano ambayo ina majukumu ya kusimamia uvuvi katika bahari kuu,”amesema.

Hata hivyo Waziri  Ulega amesema Wizara kupitia Mamlaka hiyo imefanya maboresho katika kanuni za Sheria Uvuvi wa Bahari Kuu na kupandisha utoaji wa vibali vya uvuvi katika Bahari Kuu kutoka  meli 9 mwaka 1988 hadi meli 61 mwaka 2023/24 kwa ajili ya kufanya uvuvi katika Ukanda wa Uchumi wa Bahari (EEZ) upande wa Tanzania.

Vilevile, DSFA imeingia mkataba na Kampuni ya Albacora ya nchini Hispania kwa ajili ya ujenzi wa  kiwanda cha kuchakata samaki katika Mkoa wa Tanga. Kiwanda hicho kitakuwa na uwezo wa kuchakata tani 20 za samaki kwa siku, kuhifadhi tani 2,400 za samaki na kuajiri wafanyakazi zaidi ya 100.