December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mufti wa Tanzania awataka waislam kulinda Ramadhani

Na Heri Shaaban, TimesMajira Online

MUFTI wa Tanzania Abubakari Bin ,Zuberi, aliwataka waumini wa dini ya kiislam kutumia mwezi mtukufu wa Ramadhani, kwa ajili ya kuchuma mema na kulinda Ramadhani yao.

Mfti Abubakari Zuberi, alisema hayo katika futari maalum iliyoandaliwa na Meya wa Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam Omary Kumbilamoto ambaye amewafurisha wananchi wa Dar es salaam na watoto yatima iliyoenda Sambamba kwa dua maalum la kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan.

“Nawaomba waumini wa kiislam wote Tanzania kulinda mazuri yanayofanywa na mwezi mtukufu wa Ramadhani ili Ramadhani yenu iweze kukubalika na kuyakataa mabaya yale ambayo mwenyezi Mungu anayakataa katika maandiko yake .”alisema Mufti Zuberi.

Muft Zuberi aliwataka waumini wa Kiislam kuyafanyia kazi katika miezi 11 ijayo ya Ramadhani kwani ni chuo cha waumini wa dini ya kiislam hivyo wajifunze na kuyafanyia kazi na kutenda mema .

Mufti alisema ukarimu wa Mwezi wa Ramadhani yale mazuri yanayofanywa na dini yetu yaendelee miezi yote kwa kufanya ibada na kufanya mambo mazuri anayopendeza Mwenyezi Mungu.

“Nakupongeza Meya wa Halmashauri ya jiji ukarimu huu uliofanya leo katika futari hii na kumuombea Dua maalum Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ufanyike na miezi mingine sio kwa miezi wa Ramadhani Pekee”alisema.

Alitumia fursa hiyo kwa kumuombea Meya wa Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam Omary Kumbilamoto aweze kutekeleza majukumu yake vizuri na kupanda daraja kwa kile alichotoa na Mwenyezi Mungu aweze kumzidishia .

Meya wa Halmashauri ya jiji hilo Omary Kumbilamoto aliwashukuru wananchi wa Dar es salaam kushiriki futari hiyo maalum katika Dua maalum ya kumuombea Rais ambapo futari hiyo pia wamekula watoto wa makundi maalumu ikiwemo Yatima na Wajane .

Alitumia fursa hiyo kumpongeza MUFTI Zuberi kuwa mstari wa mbele katika shughuli za Wilaya ya Ilala kwa kujitoa kwake kushiriki hasa matukio yanayoandaliwa na Ofisi ya Meya Kumbilamoto.

Meya Kumbilamoto aliwataka wananchi wa Halmashauri ya jiji hilo kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya sita ya katika miaka mitatu ya Dkt.Samia Suluhu Hassan ameweza kufungua nchi kwa fursa za kiuchumi na miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo sekta ya afya na sekta ya Elimu nchi nzima.