November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

PPRA yaokoa bilioni 16.27 mwaka 2021/23

Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

MAMLAKA ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma Nchini (PPRA)imefanya kaguzi na Chunguzi mbalimbali za Zabuni,mapambano dhidi ya rushwa kwenye taasisi za umma kwa lengo kubaini ubadhirifu na kufanikiwa kuokoa jumla ya shilingi Bilioni 16.27

Hayo yameelezwa jijini hapa leo Aprili 9,2024 na Mkurugenzi wa kujenga uwezo wa Mamlaka ya Manunuzi ya Umma PPRA, Mhandisi Amin Mcharo,wakati akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya miaka mitatu ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan Madarakani ambapo amesema kaguzi hizo zilifanywa katika kipindi cha miaka miwili cha mwaka 2021/2022 hadi mwaka 2022/2023.

Amesema Serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imeweka kipaumbele katika utafiti wenye lengo la kubaini changamoto zinazoikabili sekta ya ununuzi na kutafuta suluhisho la namna ya kukabiliana nazo.

Ambapo ameeleza kuwa katika utekelezaji wa lengo hilo, imeiwezesha Mamlaka kuandaa sera ya tafiti na agenda iliyoainisha maeneo muhimu ya kufanya utafiti katika ununuzi wa umma.

Amezitaja baadhi ya tafiti zilizofanywa na Mamlaka na kukamilika ni pamoja na tafiti kuhusu changamoto na fursa katika ununuzi wa umma ili kutatua changamoto zilizopo kwenye sekta ya ununuzi wa umma na Ushiriki wa Kampuni za biashara zinazoongozwa na wanawake katika zabuni za Umma.

Pamoja na hayo ametaja vikwazo vikubwa vinavyozuia ushiriki wa kampuni za wanawake ni kushindwa kupata dhamana ya zabuni inayotakiwa na kueleza kuwa sheria mpya imeweka mazingira ya upendeleo maalum ya kampuni hizi ikiwa ni pamoja na Mamlaka kukamilisha tafiti ndogondogo katika matumizi ya taratibu ya ununuzi kwa njia ya Force Account ambapo ilibainika kuwa kuna matumizi ya njia hii yasiyoendana na Sheria na Kanuni inavyoelekeza.

Kuhusu kujenga uwezo kwa wadau amesema
PPRA imeendesha mafunzo maalum kuhusu sheria ya ununuzi wa Umma, matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa ununuzi wa umma, mikataba na zana za kutekeleza ununuzi kwa Taasisi za Umma, wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu, makundi maalum, wazabuni na wadau mbalimbali.

“Mafunzo haya yaliyotolewa yameongeza kwa kiasi kikubwa uelewa wa sheria ya ununuzi wa umma Sura Na. 410 na matumizi ya mfumo wa kielektroniki,”ameeleza

Amesema PPRA ikiwa na dhamana ya kusimamia sekta ya ununuzi wa umma
imewezeshwa kutekeleza vipaumbele mbalimbali katika kusimamia ununuzi wa umma nchini, ambapo imeweza kutekeleza kwa mafanikio makubwa majukumu yake, ikijikita katika maeneo mbalimbali ya Ujenzi wa Mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma, kuimarisha Ufuatiliaji na Udhibiti wa Ununuzi wa Umma.

Eneo jingine ni kuwajengea uwezo wadau wa Ununuzi wa Umma, kutungwa upya kwa Sheria ya Ununuzi wa Umma Na. 10 ya Mwaka 2023, kujenga jengo la Ofisi ya Makao Makuu na kuanzishwa kwa Ofisi za Kanda ambapo katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa awamu ya sita, Serikali imetekeleza mambo mengi yanayoigusa sekta ya Ununuzi wa Umma ambayo yamekuwa na matokeo chanya kwa wadau wa sekta na kwa Watanzania kwa ujumla.

Ameeleza Katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Sita, PPRA imefanya uwekezaji mkubwa katika ujenzi wa Mfumo mpya wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma unaojulikana kama National e-Procurement System of Tanzania (NeST).

“Kabla ya uwekezaji huu, ununuzi wa umma ulikuwa ukifanyika kwa kutumia mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma uliojulikana kama Tanzania National e-Procurement System (TANePS) ambao ulijengwa na kampuni ya kigeni kutoka Ugiriki,”amesema.

Hata hivyo amesema Serikali ilibaini changamoto nyingi kwenye ununuzi uliokuwa ukifanyika kupitia mfumo wa TANePS ikiwemo taarifa zote za Ununuzi wa umma kuwa chini ya usimamizi wa kampuni ya kigeni nje ya nchi,changamoto hii na nyinginezo zilipelekea uamuzi wa kuanzisha Mfumo mbadala ambao utakuwa bora zaidi, wenye kuleta tija, unaojengwa na wataalam wa ndani na kusimamiwa na Serikali.