November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TAKUKURU, watuhumiwa rushwa CCM hapatoshi

Na Waandishi Wetu, TimesMajira Online, DSM, Mikoani

WAKATI Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikiwa kimeweka utaratibu mgumu wa kuwapata wagombea ubunge na udiwani kwa lengo ya kudhibiti vitendo vya rushwa, makada mbalimbali wa Chama hicho wameendelea kunaswa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo hivyo.

Wakati TAKUKURU ikichukua hatua hizo maeneo mbalimbali nchini, katika Wilaya ya Shinyanga Mjini, CCM imewasimamisha uongozi viongozi wake 12 wanaotuhumiwa kwa makosa ya kujihusisha na vitendo vya rushwa kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.

Kukithiri kwa vitendo hivyo miongoni mwa makada wa CCM, kumewaibua viongozi wa dini jijini Dar es Salaam jana, ambapo wamemshauri Mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli, kuendelea kusimama imara kuhakikisha anakata mfumo rushwa ndani ya Chama.

Pamoja na hatua zinazoendelea kuchukuliwa, waandishi wetu katika baadhi ya mikoa wameripoti baadhi ya matukio yanayoendelea kama ifuatavyo;

Dodoma

Mkoani Dodoma, TAKUKURU imekiri kumhoji Mbunge wa Jimbo la Mtera mkoani hapa, Livingston Lusinde maarufu kama Kibajaji baada ya kupata taarifa za Mbunge huyo kuwakusanya wajumbe wa CCM  Wilaya ya Chamwino na kuwahonga.

Mbali na Lusinde, taasisi imethibitisha kumhoji, Mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM Taifa, Halima Okashi kwa tuhuma za kutoa rushwa kwa wanachama wa CCM katika Jimbo la Mtera ili wawasaidie kwenye malengo yao ya kugombea ubunge wa viti maalumu.

Akizungumza na Majira jana Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Dodoma, Sosthenes Kibwengo, alikiri kumhoji kwa saa mbili Lusinde na baadaye kumuachia. Hata hivyo amesema uchunguzi zaidi wa tuhuma hizo unaendelea.

Kibwengo amesema ofisi yake ilipata taarifa za Mbunge huyo kuwakusanya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama wa Wilaya na Wale wa Umoja wa Wanawake Tanzania UWT wilaya ya Chamwino kwa lengo la kuwapatia fedha kwa ajili ya kuwashawishi ili wamsaidie kwenye kampeni zake za ubunge.

“Hakuwekwa ndani lakini tulimhoji kwa masaa mawili au matatu hivi, na taarifa tulizopata ni kwamba anakusanya watu na kuwahonga, hatukupata ushahidi wa yeyote kuhonga lakini uchunguzi wa hilo jambo bado unaendelea,” amesema Kibwengo.

Serukamba naye ndani

Wakati huo huo TAKUKURU imethibitisha kumshikilia aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Kigoma Kaskazini, Peter Sarukamba  kwa tuhuma za kutoa rushwa kwa wanachama wa CCM ili kushawishi mambo  yahusianayo na uchaguzi.

Kibwengo amesema kuwa Sarukamba ni mtia nia wa kiti cha ubunge na pia ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa.

Aliwataka wanasiasa wote na wananchi kujiepusha na vitendo cha rushwa ya uchaguzi kwa kuwa ni kinyume na sheria na vyombo vyote vipo makini kupambana nao.

Tabora

Mkoani Tabora, mbunge wa jimbo moja la mkoa huo kupitia CCM (jina linahifadhiwa) hivi karibuni alikamatwa na TAKUKURU akituhumiwa kutoa fedha kwa wana-CCM ofisini.

Mbunge huyo aliyemaliza muda wake alikamatwa Julai Mosi, mwaka huu saa sita mchana baada ya maofisa wa TAKUKURU kuvamia eneo la ofisi yake na kumchukua kwa ajili ya mahojiano.

Mwanasiasa huyo anadaiwa kuwaita wana-CCM watano watano ofisini kwake na kuwapatia kiasi cha fedha sh. 30,000 kila mmoja ili wamsaidie kwenye uchaguzi.

Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu hivi karibuni, Kamanda wa TAKUKURU mkoa wa Tabora, Mussa Chaaulo alikiri ‘mbunge’ huyo kushikiliwa kwa muda na kufanyiwa mahojiano na baadaye aliachiwa.

Chaulo amesema hawezi kubainisha kosa la mbunge huyo moja kwa moja, kwani suala hilo bado liko kwenye uchunguzi na litatolewa majibu ya moja kwa moja baada ya uchunguzi kukamilika.

Mwanasiasa alipolizwa kuhusiana na tuhuma hizo, alikiri kuhojiwa na maofisa wa TAKUKURU na kuachiwa baada ya mahojino hayo. Alipoulizwa kosa lake ni nini hadi akamatwe na kuhojiwa na TAKUKURU, alijibu kwamba; “Wewe andika ulichoelezwa na TAKUKURU.”

Shinyanga

Ili kuhakikisha watu wanaodaiwa kujihusisha na vitendo wanadhibitiwa, CCM wilaya Shinyanga Mjini imewasimamisha uongozi viongozi wake 12 wanaotuhumiwa kwa makosa ya kujihusisha na vitendo vya rushwa kuelekea mchakato wa uteuzi wa wagombea katika uchaguzi mkuu ujao nchini.

Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya TAKUKURU mkoani Shinyanga kuwakamata viongozi hao wakati wakijiandaa kugawana vitu mbalimbali vilivyohisiwa kutolewa kwa lengo la kuwashawishi wamchague mtu aliyevitoa.

Akitangaza mbele ya waandishi wa habari uamuzi wa kusimamishwa uongozi kwa viongozi hao jana mjini Shinyanga, Katibu Mwenezi wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Said Bwanga amesema miongoni mwa waliosimamishwa wamo viongozi wa CCM na Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) na Wazazi ngazi ya Kata na Tawi.

Bwanga aliwataja viongozi waliosimamishwa kuwa ni pamoja na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa, Asha Mwandu, Katibu Mwenezi wa CCM Kata ya Ngokolo, Zulfa Hassan na Elizabeth Benjamin ambaye ni Mwenyekiti wa UWT Tawi la Mwadui.

Waliosimamishwa wengine ni Mwenyekiti wa UWT Kata ya Ngokolo, Hulda Massaba na katibu wake, Pendo Mhapa. Pia wamo wajumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya UWT wilaya Shinyanga Mjini, Jackline Isalo, Moshi Ndugulile, Katibu UWT Tawi la Ngokolo, Elizabeth Hange naKkatibu wa Tawi la UWT, Tabu Shabani.

Wengine waliosimamishwa ni  Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya Umoja wa Wazazi wa CCM Kata ya Ngokolo, Tabu Said, Katibu UWT Tawi la Mwadui,  Happy Chikala na Katibu wa UWT Tawi la Ngokolo Shinyanga, Elizabeth Buzwizwi.

Bwanga amesema kuwa viongozi hao wote wamesimamishwa uongozi mpaka pale mashauri yao mbele ya TAKUKURU yatakapokuwa yamekamilika na kutolewa maamuzi.

Amesema Chama kitaamua ni adhabu gani watastahili kuchukuliwa kichama iwapo watapatikana na hatia.

“Maamuzi ya kuwasimisha uongozi viongozi hawa yametokana na kikao cha Kamati ya Siasa ya wilaya kilichoketi jana (juzi) ambapo tumeona siyo vyema wenzetu hawa waendelee kuwa viongozi wakati wanatuhumiwa kwa makosa ya vitendo vya rushwa,”amesema Bwanga na kuongeza;

“CCM kila siku tumekuwa tukipigia kelele vitendo vya rushwa, hasa kipindi hiki cha kuelekea vikao vya uteuzi wa wagombea nafasi za ubunge na udiwani, na hata Mwenyekiti wetu wa CCM Taifa  (Rais Magufuli) mara kwa mara amekuwa akiwaonya wana CCM wajiepushe na vitendo vya rushwa.

Viongozi wa Dini waonya

Kwa upande wao viongozi wa dini wamemshauri Mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli kusimama kidete kwa kuukata mfumo rushwa ndani ya Chama hicho badala ya kuwalinda, kwani uchaguzi wa Mwaka mwamuzi atakuwa Mwenyewe na wala siyo Tume kama ilivyozoeeleka miaka yote.

Ushauri huo ulitolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Maaskofu na Mashekhe ya Maadili, Amani na Haki za Binadamu kwa Jamii ya Madhehebu ya Dini nchini, Askofu William Mwamalanga.

“Huu ndiyo ujumbe wetu, dua yetu mbele ya Mungu kwa wote waliokumbatia mfumo wa rushwa ili wachaguliwe, tunawatumia ujumbe wetu unaosema;

“Simamia haki, tupa rushwa shimoni, kwani kwa  yeyote anayeendelea kutoa rushwa kwa lengo la kushinda uchaguzi nafasi yoyote hata kama atapitishwa kwa nguvu, ajue atatupwa shimoni na rushwa yake,” amesema Askofu Mwamalanga.

Amesema Rais Magufuli hakutoa hata senti moja ya rushwa wakati akiomba urais mwaka 2015, lakini alifanikiwa kupata nafasi hiyo, hivyo alihoji wale wanao tafuta nafasi za ubunge na udiwani kwenye chama hicho kuendeleza vitendo vya rushwa?

Akizungumza kwenye kongamano la siku mbili linalohudhuriwa na waumini 4,000 wa madhehebu ya dini mbalimbali kutoka mikoa yote nchini lililofanyika Madale nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, Askofu Mwamalanga alitaka uchaguzi wa 2020 kusimamisha haki na kuitupa rushwa shimoni.

Amesema iwapo rushwa itatupwa shimoni Watanzania watafaidi keki ya taifa ambayo imekuwa ikiliwa na kundi dogo la watu wachache katika awamu zote tangu uhuru wa nchi.

Askofu Mwamalanga alionya kuwa tayari Kamati ya Kitaifa kwa kushirikiana na waumini wa dhehebu ya dini zote inaendelea kukusanya majina ya watoa rushwa kwenye uchuguzi katika ngazi za udiwani, ubunge na urais kisha watayapeleka majina yao kwenye Dua ya kitaifa, ambapo wataomba Mwenyezi Mungu afanye kisasi juu yao wote kama njia pekee ya kuiponya nchi .

Akinukuu maandiko mbalimbali kutoka kwenye Biblia Kitabu cha Mwanzo Sura 18 Mstari wa 24 hadi 31 na Kitabu cha Kutoka Sura ya 23 mstari 8 na Mithali Sura 14 mstari wa 34, Askofu Mwamalanga amesema mistari yote hiyo inakemea rushwa.

Amesema kuwachagua watoa rushwa ni sawa na kumkataa Mungu. Naye Alhaji Hamza Kimweri na Shekhe Mwinyi Mohamed Salumu, walionya kwamba kuna watu ving’ang’anizi wa Rushwa ndani ya siasa, ambao wapo tayari kumwaga damu ili waendelee kuwa wabunge na vyeo vya kisiasa.

Kwa nyakati tofauti wamesema jambo hilo linazidi kudumaza haki na ustawi wa taifa, huku wakiua fikra pevu kwa lengo la kuendelea kulea uovu wao.

“Tunataka uchaguzi wa mwaka huu uwe huru na wa haki, bila wizi wa kura, rushwa wala mabavu ndiyo maana tunasema kauli mbiu yetu ni Simamisha Haki, Tupia Shimoni Rushwa, maana yake kila anayewaza ana hati miliki kuwa Rais, mbunge na diwani kwa kutoa rushwa ajue amepotea kwani Mungu Mwenyezi hatawaruhusu kuishi, tumechoka kukandamizwa na mfumo rushwa,” amesema mmoja wa viongozi hao.

Makada 10 watia nia

Katika hatua nyingine wanachama 10 wa CCM akiwemo mbunge anayemaliza muda wake wametangaza nia ya kugombea ubunge katika Jimbo la Shinyanga mjini.

Bwanga aliwataja wanachama waliotangaza nia hiyo kuwa ni pamoja na Stephen Masele aliyekuwa mbunge wa Jimbo hilo la Shinyanga Mjini, Erasto Kwilasa, Wilbert Masanja, Severine Kilulya, Jonathan Manyama, Lydia Pius, Mary Izengo, Dotto Joshua na Eunice Jackson.

Uchukuaji wa fomu kwa ajili ya kuomba kugombea kuteuliwa kuwa mgombea udiwani au ubunge kwa tiketi ya CCM utaanza rasmi Julai 14 hadi Julai 17, mwaka huu saa 10.00 jioni na baada ya hapo mikutano kwa ajili ya upigaji wa kura za maoni ngazi za kata na Jimbo itafanyika.

Habari hii imeandikwa na waandishi wetu mikoa ya Dodoma, Mwanza, Shinyanga, Tabora na Dar es Salaam.