November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Jiji Dodoma wataja mafaniko divisheni ya uwekezaji miaka mitatu ya Rais Dkt.Samia

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Dodoma

SERIKALI ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan imetengeneza mazingira mazuri ya uwekezaji na kuwavutia wenye viwanda kuwekeza Halmashauri ya Jiji la Dodoma na kukuza uchumi.

Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Mkuu wa Divisheni ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Abeid Msangi alipokuwa akiongelea mafanikio ya serikali ya awamu ya sita kwa kipindi cha miaka mitatu ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ukumbi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.

Msangi amesema kuwa kwa mazingira mazuri ya uwekezaji yanayofanywa na serikali ya awamu ya sita, Halmashauri ya Jiji la Dodoma itaendelea kunufaika na uchumi wake kuanza kutegemea viwanda. “Katika kwenda sambamba na ongezeko la uwekezaji katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, tumejitika kufuata maelekezo ya Mpango Kabamba wa Jiji la Dodoma.

Mpango huo umepanga maeneo kadhaa ya uwekezaji yakiwepo ya viwanda vikubwa kule Nala. Eneo la uwekezaji wa viwanda lina zaidi ya ekari 1,500 na viwanja zaidi ya 241. Sehemu ya viwanja hivyo, imetolewa kwa ajili ya ‘Export Processing Zines Authority’ (EPZA). Pia wapo wawekezaji wengine wa kati na wakubwa” alisema Msangi.

Amesema kuwa katika eneo la viwanda Nala kimejengwa kiwanda kikubwa cha mbolea Itracom chenye uwezo wa kuzalisha tani 1,000,000 za mbolea kwa mwaka. “Kiwanda hicho ni ‘icon’ kwa sasa kinazalisha tani 400,000. Kiwanda hiki kinaifanya Tanzania kuwa mzalishaji mkubwa wa mbolea na muuzaji katika soko la Afrika Mashariki na Kati.

“Kiwanda hiki kimeweza
kubadilisha kabisa uchumi wa Dodoma. Kitakapokamilika kabisa kinatarajiwa kutoa ajira rasmi zaidi ya 400 na wale wanaopata fursa kupitia kiwanda hicho kufikia 15,000,”amesema Msangi.

Mafanikio mengine amesema kuwa halmashauri inajivunia kuanza kujengwa kiwanda kingine kikubwa kitakachokuwa kinazalisha na kuchuja mbegu za mafuta ya alizeti, ufuta na karanga.

”Kiwanda kinajengwa eneo la Veyula na kitakuwa na uwezo wa mchujo mara mbili. Kiwanda kitaweza kukamua alizeti tani 200 kwa siku na kuzalisha mafuta yenye mchujo mara mbili tani 100 kila siku,Kiwanda kikikamilika kitaweza kuajiri wafanyakazi kati ya 500-600,”amesema Msangi.

Msangi amesema “ndani ya miaka mitatu tumeshuhudia mabadiliko makubwa, mfano leseni za viwanda vidogo zimebadilika zaidi ya mara mbili katika kipindi cha miaka mitatu. Tulitoa leseni 242 mwaka 2020 hadi kufikia mwisho wa mwaka 2023 tumetoa leseni za viwanda vidogo 582.

Yote hii inaonesha mazingira bora yaliyojengwa na serikali ya awamu ya sita yameweza kuvutia uwekezaji katika hii sekta lakini pia kuongeza nafasi za ajira na kuongeza pato la taifa”.

Halmashauri ya Jiji la Dodoma imefanya jambo kubwa katika kutambua mchango wa machinga. Halmashauri imetambua machinga zaidi ya 3,000 na kuwajengea soko kubwa kwa shilingi bilioni 9.5 na mazingira yao ya kufanya biashara ni mazuri na salama, aliongeza.