Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online DSM
CHAMA cha Skauti Tanzania (TSA) kimemsimamisha aliyekuwa Mkufunzi wa Chama hicho Faustine Magige na kumfuta hadhi ya kuwa Mkufunzi msaidizi wa chama na kumtaka mara moja kuacha kutumia jina la Skauti katika shughuli zozote za chama hicho, Pia TSA imemsimamisha kiongozi wa kundi Festo Mazengo kutofanya shughuli zozote za Skauti mpaka pale mkutano mkuu wa Skauti utakapoamua vinginevyo.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Makao Makuu ya Skauti Upanga Dar es Salaam, Kamishna Mkuu wa Chama cha Skauti Tanzania Abubakari Iddi Mtitu amesema maamuzi hayo yamefanyika baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya wazazi wa vijana wa Skauti ambao walitarajia watoto wao waweze kusafiri safari za kieleimu nje ya Nchi ambao walichanga pesa zao na kiongozi huyo kuwahadaa wazazi hao kwa kuweka katika akaunti binafsi wakati akijua wazi kuwa ni kinyume cha miongozi ya chama hicho kinachowtaka wazazi kuweka katika akaunti rasmi ya Kundi au Wilaya
“Kama mnavyofahamu Faustin Gervas Magige amezua mgogoro kati yake na baadhi ya Wazazi wa Skauti ambao wanamdai baada ya kuingiza fedha za safari ya skauti kwenye akaunti ya kampuni binafsi ya Faustin Magige, iitwayo DAR ES SALAAM SCOUT BUREAU (DSB). Safari hiyo ilikuwa ni ya Kundi la Skauti la shule ya IVY First Pre & Primary School iliyopo Kigamboni, linaloongozwa na Festo Mazengo na safari ilipaswa kufanyika mwezi Disemba, 2023 kuelekea Afrika ya Kusini lakini si wanafunzi wote walifanikiwa kusafirishwa”. amesema
Aliongeza kuwa Chama kilipokea Malalamiko ya Mzazi mwingine mwenye mtoto katika Shule ya St. Joseph Millenium, ambae anadai arudishiwe fedha zake kwa vile hawakufanikiwa kumsafirisha katika safari ya Uturuki mwezi April 2023, kama msindikizaji. Malalamiko hayo yanamhusu Faustin Magige ambae alipokea fedha kiasi cha TZS 4,000,000/= kupitia akaunti ya kampuni yake binafsi ya DAR ES SALAAM SCOUT BUREAU (DSB) ilhali kiongozi wa kundi la skauti la St. Joseph Millenium, Vicent Magige aliishafunga orodha ya wasindikizaji wawili waliopitishwa na shule.
Baada ya Chama cha Skauti kupokea malalamiko hayo, Uongozi wa Chama kwa mujibu wa Katiba (2017) Ibara ya 10.6.2 (vi) inahusu maamuzi yanayochukuliwa dhidi ya Kiongozi anayekwenda kinyume na matakwa ya Chama na kwa kutambua hatua walizochukuwa baadhi ya wazazi kwa kumfungulia kesi Faustin G. Magige ili wapatiwe haki zao, Chama kilichukua hatua za haraka na kuwasiliana na Faustin G. Magige ili kuona uwezekano wa kutatua tatizo hilo pasipo kuathiri shughuli za Chama, ikiwa ni pamoja na kusitisha kwa muda safari za kielimu na mafunzo nje ya nchi, ili kufanya maboresho katika taratibu za safari zinazoandaliwa na Viongozi wa makundi ya Skauti katika ngazi za Wilaya.
Hivyo, Kwa mujibu wa Sera, Muundo na Sheria (SMS) ya mwaka 2019 kipengele na. 60 (ii) kinasema Fedha zote zinazopatikana kwa ajili ama kwa niaba ya Chama lazima zilipwe kwenye akaunti ya benki yenye jina la kundi ama Baraza husika (council) inayoendeshwa na watia saini walioidhinishwa kwa ajili hiyo wasiopungua wawili.
Pamoja na juhudi za awali Bodi ya Skauti Taifa kupitia Kikao chake cha Tarehe 08/03/2024 ilijadili na kuazimia yafuatayo:
i.Kuwasimamisha Faustin Magige na Festo Mazengo wasifanye shughuli zozote za Skauti hadi Tarehe ya Mkutano Mkuu ili kupata hatma yao kwa kufanya makosa ya kukitia aibu Chama, kutokuwa waaminifu na kutozingatia Taratibu za Chama.
ii.Faustine Magige asitishe mara moja matumizi ya neno “SCOUT” katika jina la biashara / kampuni yake binafsi kwani ni kinyume na Katiba, Sera, Mwongozo na Sheria ikizingatiwa yeye ni Skauta anauelewa wa kutosha kuhusiana na kosa hilo. Kwa kosa hili amekiuka SMS (2019) kipengele na.31.1&31.2 Ulinzi wa jina na nishani kinasema, “utambulisho wa nishani ya Skauti ya ulimwengu nembo, nishani na neno “SCOUT” havitatumika nchini Tanzania kwa ajili ya kujitangaza, matangazo ya biashara isipokuwa kwa makubaliano ya kimaandishi baina ya Makao Makuu na Shirika husika”.
iii.Kamishna Mkuu atumie mamlaka yake ya kikatiba na kushirikisha vyombo vyake vya maamuzi/ushauri afute hati (warrant) ya Faustin Magige na kumwondolea hadhi ya Mkufunzi Msaidizi.
iv.Kamishna Mkuu, ndani ya miezi mitatu, aboreshe utaratibu wa kuratibu safari za kielimu na mafunzo za Skauti Nje ya nchi ambao kila kiongozi wa kundi atapaswa kufuata kinyume na hapo, hatopewa kibali cha safari na anaweza kufungiwa.
v. Kamishna Mkuu aondoe zuio lililotolewa kupitia barua ya Tarehe 06 Februari, 2024 kwa Kumb. Na. TSA/INT/131/02 kuhusu kusitishwa kwa safari za nje ya nchi mara baada ya kukamilisha maboresho ya taratibu za safari za nje ya nchi. Kwa maelekezo kwamba, Programu za safari za nje ya Nchi ngazi ya makundi zitaanza rasmi kufanyika baada ya miezi mitatu tangu sasa, iwapo taratibu husika zitakuwa zimeishakamilishwa na Kamishna Mkuu, nakuanza rasmi mwezi Juni, 2024.
kwa niaba ya Skauti Tanzania nichukue nafasi kuwaomba radhi sana wazazi na wadau waliopata changamoto hii, ambayo kwa kiasi kikubwa inaweza kuchafua jina la Skauti Tanzania, Chama ambacho kimekua kikifanya kazi zake kwa weledi mkubwa. Aidha, niwatake Viongozi wa Makundi, Makamishna wa Wilaya na Mikoa kusimamia utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Bodi. Chama cha Skauti kinaahidi kwamba, kitaendelea kusimamia utolewaji wa huduma na shughuli za Skauti kwa manufaa ya Vijana na Umma.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa