November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mahundi azindua uchimbaji  visima vya maji

Na Esther Macha,TimesmajiraOnline, Mbarali

NAIBU Waziri wa Maji ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mbeya, Mhandisi Maryprisca Mahundi amezindua mradi wa uchimbaji visima vya maji kwa kata tano zilizopo Wilayani Mbarali zitanufaika na mradi huo .

Uzinduzi wa mradi huo umefanyika katika Kijiji cha Azimio Mapula Kata Kongolo Mswiswi Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya na kwamba visima vingine vitachimbwa katika vijiji vya Mpolo,Uwalanje ,Ibohola,Limsemi,Nyakazombe pamoja na Vikaye.

Aidha Mhandisi Mahundi amesema kuwa Wizara itakamilisha kiasi cha shilingi mil. 96 hivi karibuni ambazo lengo lake ni kuukamilisha mradi huo ili mitambo iweze kuhamia Kata zingine nao waonje keki ya Mama Samia Suluhu Hassan.

Meneja wa RUWASA Wilaya ya Mbarali Mhandisi Samwel Heche amesema mpaka sasa visima ishirini vimechimbwa Mkoani Mbeya tangu kuwasili mtambo huo Mkoani Mbeya na mradi wa Azimio Mapula ukikamilika utagharimu mil 107,352,742/- mpaka sasa zimetumika mil 10,400,000/- ili mradi ukamilike zinatakiwa mil.96,952,742 na kuomba Wizara kukamilisha fedha hiyo kukamilisha mradi.

Mkuu wa Wilaya ya Mbarali Kanali Denis Mwila mbali ya kuwataka wananchi kutunza miundombinu ya maji na vyanzo vya amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ,Waziri wa Mji,Naibu Waziri wa Maji kwa kutatua kero ya maji.

Aidha Diwani wa Kata ya Mswiswi Eliah Bange amemshukuru Naibu Waziri wa Maji kwa kutatua kero ya maji katika vitongoji vyote vitano vya Kata hiyo.

Bange ameitumia nafasi hiyo kuiomba RUWASA kuboresha baadhi ya miundo mbinu ya maji katika kata yake ambayo mingi imechakaa na ongezeko la watu limefanya maji kushindwa kutosheleza wakazi wa Kata ya Mswiswi.

Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Mbarali Zabibu Nuroo ameishukuru Serikali kwa kutekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya kuhakikisha inamtua mama ndoo kichwani.

Uzinduzi wa uchimbaji visima vya maji Wilaya ya Mbarali umeendana na maadhimisho ya wiki ya maji duniani yaliyoanza machi 16,2024 na kilele chake ni machi 22,2024.