November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kamati Kituo cha Dkt. Salim Ahmed Salim yazinduliwa

Na Mwandishi wetu,TimesmajiraOnline,Dar

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba, amezindua Kamati ya Kupitia Majukumu na Maboresho ya Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim.

Kamati hiyo itakayofanya tathmni ya kina ya majukumu ya Kituo na kuanisha maeneo yanayohitaji maboresho ili kuwa na kituo chenye kukidhi mahitaji ya wadau wake kwa mahitaji ya sasa na ya kikazi kijacho.

Rais Samia Suluhu Hassan aliunda Kamati ya kufanya Tathmni ya Utendaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki pamoja na taasisi zilizo chini ya Wizara ikiwemo Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim, ambapo pamoja na mambo mengine kamati ilipendekeza umuhimu wa kufanyika tathmini ya kina na kufanya mabadiliko makubwa katika Kituo kwa lengo la kuwa na Taasisi ya Mafunzo ya Kitaaluma, Utafiti na Stadi za Kidiplomasia na pia kuwa Kituo rejea cha fikra (Think Tank).

Mwenyekiti wa Kamati, Balozi Hamis Kagasheki

Kituo cha Dkt. Salim tayari kimesaini Hati za Makubaliano na Taasisi kutoka nchi za Algeria, Angola, Afrika Kusini na Umoja wa Falme za Kiarabu.

Kituo pia kimeingia makubaliano na Chuo cha Usimamizi wa Mahakama, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Chuo cha Utawala wa Umma, Chuo cha Taifa cha Ulinzi, na Mpango wa Hiyari wa Kujitathmini Wenyewe (APRM) ambapo kamati hii itaangalia utekelezaji wa Hati hizo za Makubaliano na kuanisha maeneo ambayo yanahitaji msukumo na maboresho ili kuleta manufaa yaliyokusidiwa.

Kamati hii ina wajumbe nane ikiongozwa na Mwenyekiti Balozi Khamis Kagasheki na wajumbe wengine akiwemo Balozi Dkt. Ramadhan Dau, Dkt. Salim Hamad, Prof. Marcellina Chijoriga, Dkt. Lucy Shule, Dkt. Godfrey Sansa, Dkt. Kadari Singo, na Dkt. Asumpta Muna

Aidha, Mwenyekiti wa Kamati, Balozi. Kagasheki alisema kamati itasimamia vyema majukumu iliyopewa na kupendekeza pale itapoona uhitaji wenye tija zaidi hata ya majukumu vipengele vya sasa.

Awali, Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim kilijulikana kama Kituo cha Mahusiano ya Kigeni cha Msumbiji na Tanzania, au Kituo cha Mahusiano ya Kigeni (CFR).